NA MWANDISHI WETU, DAR ES SALAAM
KAMATI ya Maadili ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), imewafungia maisha kujihusisha na mpira wa miguu wanafamilia wawili wa mchezo huo kwa madai ya kuhusika na upangaji matokeo.
Taarifa iliyotolewa na TFF leo imewataja waliofungiwa ni kocha Ulimboka Mwakingwe na Mwenyekiti wa Kitayosce FC Yusuph Kitumbo.
Taarifa hiyo imeeleza kuwa wadau wa hao wa soka wametiwa hatiani kwa kosa la upangaji matokeo katika ligi ya Championship, ambapo wawili hao walipaswa kufika mbele ya kamati hiyo lakini Kitumbo hakufika wala kutoa udhuru, huku Mwakingwe akiwasilisha utetezi wake kwa njia ya maandishi.
Taarifa zinaeleza kuwa Kitumbo na Mwakingwe walijihusisha na upangaji matokeo katika mchezo wa Championship kati ya Fountain Gate Fc na Kitayosce uliochezwa Aprili 29 mjini Morogoro.