NA MWANDISHI WETU, DODOMA
SERIKALI imesema taasisi za uhifadhi nchini zimeendelea kutekeleza majukumu yake ipasavyo kufuatia muundo wa sasa wa Jeshi la Uhifadhi kuziwezesha taasisi hizo kufanya kazi zake vizuri.
Hayo yamesemwa leo Mei 4, 2023 Bungeni jijini Dodoma na Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mary Masanja kwa niaba ya Waziri wa Maliasili na Utalii alipokuwa akijibu swali la Mbunge wa Malinyi, Antipas Mgungusi aliyetaka kujua lini Jeshi la Uhifadhi litapata Kamishna Jenerali ili kukamilisha muundo wa kijeshi na kuleta muunganiko katika divisheni ya Mamlaka ya Uhifadhi ya Ngorongoro (NCAA), Shirika la Hifadhi za Taifa Tanzania (TANAPA), Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania (TAWA) na Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS).
Akijibu swali hilo Naibu Waziri Masanja amesema kuwa muundo wa Jeshi la Uhifadhi umefanya taasisi hizo kufanya kazi zake vizuri huku kila moja ikiwa inasimamiwa na Kamishna wa Uhifadhi.
“Taasisi hizi zina majukumu tofauti kwa mfano TAWA na TFS zinaruhusu uvunaji na uwindaji wa kitalii, tofauti na TANAPA na Mamlaka ya Hifadhi ya Eneo la Ngorongoro (NCAA),” amesema Masanja
Amesema taasisi hizo zinafanya kazi vizuri na zote zinaripoti kwa Katibu Mkuu Wizara ya Maliasili na Utalii na kufafanua kuwa endapo kutabainika kuwa na changamoto katika utekelezaji wa mfumo huo, Serikali itafanya marejeo ya sheria ya wanyamapori ili kuwezesha kuwa na Kamishna Jenerali wa Jeshi la Uhifadhi wa wanyamapori na misitu.