NA MWANDISHI WETU, ZANZIBAR
Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Wanawake, Jinsia, Wazee na Watoto wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ), Riziki Juma ametoa wito kwa wadau wa elimu kuhamasisha wanafunzi wa kike kupenda kusoma masomo ya sayansi, teknolojia na hisabati.
Wito huo ameutoa Mei 3, 2023 katika hafla ya kusaini makubaliano ya uendelezaji wa wanawake katika sekta ya nishati iliyofanyika katika hoteli ya Madinat Al Bahar – Zanzibar ambapo Taasisi ya Teknolojia Dar es Salaam (DIT) imeingia makubaliano hayo ikiwa ni miongoni mwa taasisi zitakazo zitatoa mafunzo.
Mradi wa uendelezaji wanawake walioajiriwa (in-service employees) na wale waliomaliza masomo ambao hawajaajiriwa (internship) unafadhiliwa na Benki ya Dunia na kusimamiwa na Wizara ya Maji, Nishati na Madini na kuratibiwa na Zanzibar Energy Sector Transformation and Access Project (ZESTA).
Katika utekelezaji wa mradi huu inatarajiwa kwamba takriban wanawake 115, kati yao wanawake 15 walioajiriwa na wanawake 100 waliohitimu masomo yao na hawajaajiriwa watanufaika na mpango huu wa uendelezwaji.
Lengo kuu la uendelezaji wanawake hawa ni kuwajengea uwezo kitaaluma ili waweze kushika nafasi na nyadhifa mbalimbali za uongozi katika sekta ya nishati.
Katika hafla hiyo Wizara ya Maji, Nishati na Madini ya Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ) imesaini makubaliano na Taasisi tano za elimu ya juu ambazo ndizo zitatoa mafunzo hayo. Taasisi hizo ni Chuo Kikuu cha Zanzibar (ZU), Chuo Kikuu cha Taifa Zanzibar (SUZA), Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Taasisi ya Teknolojia Dar es Salaam (DIT) na Taasisi ya Sayansi na Teknolojia ya Karume (KIST).