NA MWANDISHI WETU, DODOMA
TAKWIMU za Shirika la Kazi Duniani (ILO) zilizotolewa katika kipindi cha mwaka 2022, zinaonesha kuwa watu milioni 2.9 walipoteza maisha kutokana na ajali na magonjwa yatokanayo na kazi.
Pia, zaidi ya wafanyakazi milioni 402, huumia wakiwa kazini na hivyo kushindwa kutekeleza majukumu yao kwa kipindi chote wanachopatiwa matibabu.
Hayo yamesemwa leo Aprili 26,2023 jijini Dodoma na Waziri wa Nchi Ofisi ya waziri mkuu Kazi,Vijana, Ajira,na Wenye ulemavu Prof. Joyce Ndalichako, wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu maandalizi ya maadhimisho ya siku ya Afya na Usalama Mahala pa kazi kitaifa yatakayofanyika mkoani Morogoro.
Prof.Joyce Ndalichako amesema Kwa upande wa Tanzania jumla ya ajali na magonjwa yaliyoripotiwa katika Mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi kuanzia Julai 2019 hadi Juni 2021 ni ajali 4,993 na magonjwa 249. Katika ajali hizo, vifo vilikuwa 217.
“Takwimu hizo ni kubwa sana zinaathiri utendaji kwa kuwa zinasababisha upotevu wa maisha ya Wafanyakazi na pia kuathiri shughuli wakati wafanyakazi walioumia wakiendelea kupata matibabu. Kwa mantiki hiyo, ni dhahiri kwamba suala la ajali na magonjwa yatokanayo na kazi linahitaji jitihada za makusudi katika kukabiliana nalo,”
“Kupitia Taasisi yake ya OSHA serikali inaendelea kusimamia kwa karibu utekelezaji wa sheria Na. 5 ya Afya na Usalama Mahali pa Kazi ya mwaka 2003 miongoni mwa wadau na Watanzania wote kwa ujumla”amesema
Aidha amesema kuwa takwimu hizo ni kubwa na zinaathiri utendaji kwa kuwa zinasababisha upotevu wa maisha ya wafanyakazi na pia kuathiri shughuli wakati walioumia wakiendelea kupata matibabu.
“Kwa mantiki hiyo, ni dhahiri kwamba suala la ajali na magonjwa yatokanayo na kazi linahitaji jitihada za makusudi katika kukabiliana nalo serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inatambua umuhimu wa kulinda nguvu kazi ya Taifa.
“Tunapoelekea kilele cha maadhimisho ya siku ya Usalama na Afya mahali pa Kazi tarehe 28 Aprili 2023, serikali kwa kushirikiana na wadau wetu wa utatu tunaendesha kampeni maalum ya uhamasishaji kupitia shughuli za mafunzo ya Usalama na Afya miongoni mwa makundi mbali mbali wakiwemo wajasiriamali wadogo, wafanyakazi wa viwandani, wachimbaji wadogo pamoja na watu wenye ulemavu”amesema
Prof.Ndalichako amesema kuwa maadhimisho hayo yatafanyika kitaifa Mkoani Morogoro katika viwanja vya Tumbaku Aprili 28,2023
Kwa upande wake Mtendaji Mkuu wa OSHA, Khadija Mwenda amesema kuwa moja kati ya eneo ambalo ajali nyingi zinaripotiwa ni katika sekta ya Uzalishaji ambapo imeajiri vijana wengi huku wengine wakiwa hawana ujuzi wa kutosha katika nafasi wanazofanyia kazi.
“Ukweli ni kwamba eneo la Uzalishaji lina matukio mengi ya ajali na hii ni kutokana na vijana wengi kujikita katika eneo hilo kujiajiri ama kuajiriwa huku wengine wakifanya tu bila kuwa na ujuzi wa kutosha au taaluma kwani eneo hilo mara nyingi wanaangalia nguvu sana kuliko taaluma ndio maana ajali zinakuwa nyingi,” amesema Mwenda
Mwenda amesema kuwa OSHA imejipanga vyema kuelekea maadhimisho hayo ya 19 ambapo washiriki wote watapatiwa Mafunzo ya Usalama na Afya miongoni mwa makundi mbali mbali wakiwemo wajasiriamali wadogo, wafanyakazi wa viwandani, wachimbaji wadogo pamoja na watu wenye ulemavu.
“Pia OSHA tutajikita katika kutoa mafunzo kwa Sekta binafsi na zile zisizo rasmi kwa sababu wengi hawapo kwenye mfumo jambo ambalo linawafanya kuwa katika mazingira hatarishi na kufanya kazi bila kuzingatia sheria za usalama na afya mahali pa kazi,”amesema Mwenda
Naye Rais wa Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi Tanzania (TUCTA),Tumaini Nyamhokya ameiomba serikali kuweka sheria kali zilizopo ili ziweze kuwabana waajiri katika kuhakikisha kunakuwa na usalama mahali pa kazi.
Mwakilishi wa Shirika la kazi Duniani (ILO), Getrude Sima amesema wataendelea kushirkiana na serikali ya Tanzania
Siku ya usalama mahala pa kazi duniani ilianza kuadhimishwa mwaka 1996 nchini Marekani ambapo waathirika na watu walioumia na kupoteza maisha wakiwa kazini hukumbukwa ambapo kwa Tanzania ilianza kuadhimishwa mwaka 2004.
Kauli mbiu ya mwaka huu inasema Mazingira salama na afya kazini ni kanuni na haki ya msingi mahali pa kazi