NA ANDREW CHALE,DAR ES SALAAM
BENKI Kuu ya Tanzania (BoT) imebainisha kuwa uaminifu na urejeshaji wa mikopo kwa wakati una nafasi kubwa ya kusaidia riba za mikopo nchini kupungua.
Hayo yamebainishwa Aprili 25,2023 na Mkurugenzi wa Utafiti na Sera za Uchumi wa Benki kuu, Dk. Suleiman Missango wakati wa semina ya siku moja juu ya uelewa wa Sera ya Fedha kwa Waandishi wa Habari Wanachama Klabu ya Waandishi wa Habari Dar es Salaam (DCPC).
Dk. Missango amebainisha kuwa, kumekuwa na lalamiko juu ya uwepo wa riba kubwa mara kwa mara ambapo amebainisha kuwa, endapo jamii ya Watanzania watatoa taarifa sahihi kwa vyombo vya kutoa mikopo basi suala hilo la riba kuwa kubwa litapungua.
Amebainisha kuwa, Sera ya fedha inalenga kuweka mazingira wezeshi kwa ajili ya shughuli ya kiuchumi ikiwemo biashara, uwekezaji, lakini pia shughuli hizo za uchumi zinahusu pamoja na mikopo.
Amesema, mikopo pia ni shughuli za uchumi, ikiwemo kutoka kwenye taasisi za kifedha ikiwemo benki na pia kwenda sekta zingine.
“Shughuli za uchumi zinahusu hata mikopo ili ziweze kuendelea.
Wawekezaji wanakuwa na fedha kwa ajili ya kuwekeza na fedha hizi zingine zinatoka kwenye mikopo, ambazo mikopo hii inatoka kwenye benki.
Mikopo kwenda kwenye sekta binafsi ambapo kumekuwepo na malalamiko kwamba riba ipo juu.
Tanzania ilipotoka kulingana na nchi zingine tunazofanana nazo kiuchumi tumeona riba zetu zipo juu, Lakini ni sisi tupo nafuu kuliko nchi hizo ambazo tunafananao” amesema Dk.Missango
Aidha, amesema ukiangalia miaka ya nyuma tulipotoka unaona kabisa riba zimekuwa zikishuka lakini hazijafika pale ambapo tunataka.
“…Kulingana na mwenendo wa uchumi, tunadhani kwamba bado kuna nafasi ya kuweza kupunguza riba kutoka pale zilipo” amesema Dk. Missango.
Aidha, amesema, kumekuwa na sababu mbalimbali zinazofanya riba iwe juu ikiwemo baadhi ya wakopaji kutokuwa waaminifu katika mikopo katika vyombo vinavyotoa mikopo hiyo.
“Jamii yetu tushirikishane kuhakikisha kwamba tunapoenda kukopa kwenye taasisi za fedha tuweze kutoa taarifa sahihi ili kuziwezesha hizo taasisi ziweze kuchakata vizuri mikopo hiyo na kuhakikisha vile viashiria vya kutolipa mikopo vinakuwa vinapungua kwa kiasi kikubwa sana”
“Wanahabari ni muhimu sana katika kutoa taarifa hii kuwafikia jamii ilikuwaweze kuwa waaminifu katika mikopo yao.” amesema Dk. Missango.
Katika hatua nyingine amesema Benki Kuu katika kukomesha suala la mikopo chechefu, wameweka utaratibu wa kuchukuliwa hatua kwa wanaobainika.
“Tayari Benki Kuu imechukua maamuzi kwa Wafanyakazi wote wa sekta za kibenki ambao sio waaminifu wanaosababisha mikopo chechefu” amebainusha na kuongeza kuwa
“Watakaobainika ni kuwaondoa utumishi wao na kuwaweka kwenye kundi la kitabu cheusi ‘Blacklist’ ili wafanyakazi kama hao wasiingie tena kufanya kazi kwenye sekta ya fedha hapa nchini.”
Aidha ameeleza kuwa taasisi za kifedha mara nyingi inahusisha vipato vya watu, hivyo tunahitaji uwaminifu wa hali ya juu na lazima tuhakikishe tunakuwa na nidhamu.
Hata hivyo Dk. Misango amesema kuwa, ili uchumi uendelee kukua, Wananchi wametakiwa kupeleka fedha zao benki ili fedha hizo ziwezeshe maendeleo.