NA DENIS SINKONDE ,SONGWE
MWENYEKITI wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Kata ya Mlowo Wilayani Mbozi Mkoani Songwe, Meshack Mwambogolo amekutwa amejinyonga katika msitu uliopo kitongoji cha Iyenga Kijiji cha Shaji Kata ya Mlangali baada ya Rafiki yake aitwaye Joseph Muhume ambaye wanafanya naye biashara pamoja kutoroka na Sh. Milioni 118.
Kamanda wa Polisi mkoani hapa, Theopista Mallya amesema mwili wake umekutwa ukiwa unaning’inia kwenye mti leo Aprili 24, 2023 asubuhi ambapo alijinyonga kwa kamba ya manila huku akiacha ujumbe kuwa Familia yake imsamehe kwa maamuzi aliyofanya.
Kamanda Mallya amesema jana Mwambogolo alitoa sh. Milioni 118 na kuziweka kwenye akaunti ya Joseph Muhume kwa ajili ya kununulia kahawa ambapo baada ya kumuingiza fedha hizo Joseph alitoroka.
“Baada ya Mwambogolo kupewa taarifa kuwa Joseph ametoroka alichukua kamba na chupa ya sumu ya kuulia wadudu na kutoweka ndipo mwili wake ulikutwa asubuhi ukiwa unaning’inia kwenye mti huku akiwa ameacha ujumbe ambao unaiomba familia yake imsamehe kwa uamuzi alioufanya wa kujinyonga”
Katibu wa CCM mkoa wa Songwe, Juma Mpeli amesema wamepata taarifa hiyo ambayo imewasikitisha huku taratibu nyingine zikiwemo za kipolisi zikiendelea.