NA MWANDISHI WETU, RUNGWE
KATIKA kuelekea kilele cha Maadhimisho ya miaka 59 ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar Aprili 26, 2023, Mkuu wa wilaya ya Rungwe , Jaffar Haniu amezindua rasmi zahanati ya Isyonje iliyopo kata ya Isongole.
Pamoja na uzinduzi wa zahanati hiyo pia ameongoza wakazi wa kijiji hicho zoezi la upandaji miti ikiwa ni hatua muhimu ya kuhifadhi mazingira na utunzaji wa uoto wa asili.
Akizindua zahanati hiyo , Haniu amewashukuru wakazi wa kata hiyo kwa utekelezaji mzuri wa miradi ya maendeleo na Kuwa hatua hiyo itasaidia kuwasogezea huduma za kijamii kwa ukaribu zaidi.
Amesema serikali katika kuunga mkono juhudi za wananchi imeendelea kutoa fedha kwa ajili ya Ukamilishaji wa miradi ya maendeleo akiuangazia Mradi huo ambao umenufaika na kiasi cha shilingi Milioni 50 kwa ajili ya ukamilishaji.
Zahanati hii pia imenufaika na Vifaa tiba vyenye thamani ya shilingi million 25 , fedha iliyotolewa na serikali ya Jamuhuri ya Mungano wa Tanzania inayoongozwa na Rais Dk.Samia Suluhu Hassan.
Aidha amewataka wakazi wa kata hiyo kuepuka migogoro mbalimbali ambayo imekuwa ikirudisha nyuma maendeleo.
Haniu ametoa maelekezo kwa wananchi kujenga tabia ya kumaliza tofauti zao katika ngazi ya kaya hali itakayosaidia kupanua wigo wa amani na ustawi wa jamii kwa ujumla.
Katika hatua nyingine Haniu ameendelea kuwambusha wakazi wa wilaya ya Rungwe kutoa elimu ya malezi na makuzi kwa vijana ili kuwasaidia kujiepusha na vitendo viovu yakiwemo mapenzi ya jinsia moja, wizi, na jinai nyingine nyingi.