NA MWANDISHI WETU, MBEYA
JESHI la Polisi mkoani Mbeya limesema litaanza kuwachukulia hatua wananchi wanaokaidi kutii sheria za nchi kwa kutokuwa na utayari wa kusimama na kuimba wimbo wa taifa kwenye shughuli za kiserikali.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mbeya, Benjamin Kuzaga amesema leo Ijumaa Aprili 21, 2023 ikiwa ni siku moja baada ya maadhimisho ya Wiki ya Nenda kwa usalama barabarani baada ya kushuhudia wananchi wakiendelea na shughuli za kiuchumi wakati bendi ya Jeshi la Magereza wakiongoza wimbo wa Taifa, huku askari viongozi wa Serikali wakionyesha ishara ya kuheshimu.
“Nilikuwa nimefikilra kwa wakati ule kutoa agizo kwa askari kuwakamata wananchi waliokiuka sheria za nchi kwa kudharau wimbo wa taifa huku viongozi wakitii, lakini nimeona ni vyema kutoa maelekezo kwani kitendo kile ni kudharau nembo ya taifa,”amesema.
Kuzaga amesema ni jambo la kushangaza Jimbo la Mbeya Mjini linasimamiwa na kuongozwa na Spika wa Bunge, Dk Tulia Ackson anayesimamia sheria sasa inapotokea wananchi kutotii sheria za nchi inatengeneza taswira mbaya katika jamii.
“Nitoe wito kwa wananchi kutii sheria za nchi kwa kusimama pindi wanaposikia wimbo wa Taifa au bendera ya Taifa kushushwa vinginevyo sasa hatua zinaanza kuchukuliwa ili kuwakumbusha nidhamu ya nembo ya taifa,”amesema.
Awali Mkuu wa Wilaya ya Mbeya, Beno Malisa amelipongeza Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya kwa kutekeleza maelekezo ya Waziri Mkuu Kassim Majaliwa wakati wa maadhimisho ya Wiki ya Nenda kwa Usalama Barabarani yaliyofanyika kitaifa Mkoa wa Mwanza.
“Waziri Mkuu alitoa maelekezo ya kufanyika Wiki ya Nenda kwa Usalama barabarani nchi nzima hiyo inaonyesha ni jinsi gani kamati iiyoundwa kuratibu inavyozingatia maelekezo ya viongozi wakuu wa nchi,”amesema.