NA MWANDISHI WETU, KATAVI
JESHI la Polisi mkoani Katavi katika kipindi cha Aprili 2023 limekamata watu 24 wakituhumiwa kwa makosa tofauti ikiwamo kujihusisha na vitendo vya wizi, ujangili, kumiliki silaha kinyume cha sheria na madawa ya kulevya.
Akizungumza na wanahabari Kamanda wa Polisi Mkoa wa Katavi, ACP Ally Makame leo Aprili 21, 2023 amesema watu hao wamekamatwa kupitia misako na operesheni.
Amesema watuhumiwa wawili Benedict Gasper (32) mkazi wa Majengo na Fideris Ruben (29) mkazi wa Airtel wakituhumiwa kuiba pikipiki mbili moja ni aina ya Honlg na nyingine ni Sanlg mali ya Robert Ismail.
Aidha amesema watuhumiwa Nahimana Charles (59) na Emmanuel Benedictor (45) Wakazi wa Katumba wamekamatwa na silaha aina ya gobore wakiitumia katika shughuli za uwindaji haramu kinyumbe cha sheria.
“Tumemkamata pia Gabriel Deogratius (42) Mkazi wa Kawajense akiwa na nyara za serikali ambayo ni nyamapori aina ya nyati kilo 45 iliyokuwa imehifadhiwa kwenye mfuko chumbani kwake,” amesema.
Sanjari na hayo amesema wapo watuhumiwa 9 waliokamatwa kwa makosa ya jinai na wamefikishwa mahakamani na kufungwa vifungo tofauti.
Amewataja watuhumiwa hao kuwa ni Geofrey Patrick na John Marashi walijihusisha na kosa la kuvunja nyumba na kuiba na Hussein Omary na wengine wanne waliingia pori la akiba na kupatikana na mazao ya mistu bila kibali.
“Joseph Thomas na wenzake watatu walijifanya watumishi wa serikali na kujipatia fedha kwa njia ya udanganyifu.
Hata hivyo amesema kuelekea sikukuu ya Eid el Fitri wamejipanga kuimarisha ulinzi na yeyote atakayevunja Sheria atakamatwa na kufikishwa kwenye vyombo vya Dola