NA MWANDISHI MAALUM, KOROGWE
WAZIRI wa Maji Jumaa Aweso amemuondoa Mkurugenzi Mtendaji wa Mamlaka ya Maji ya Korogwe Sifael Masawa na kumuelekeza Katibu Mkuu Wa Wizara ya Maji Mhandisi Nadhifa Kemikimba kumpa nafasi Masawa kwenda kusoma ili kuongeza elimu na ufanisi katika utaalamu wa masuala ya Maji.
Aidha Waziri Aweso ameelekeza kuondolewa kwa Mkandarasi anaetekeleza mradi wa Maji wa Goha-Mkumbala Korogwe vijijini kutokana na kusuasua kumaliza utekelezaji wa Mradi huo na kazi isiyoridhisha.
Pia ameelekeza Mamlaka ya Maji Korogwe kuwa chini ya uangalizi kwa Mhandisi Yohana Mgaza ambae anasimamia mradi wa Maji wa Kimkakati wa kitaifa wa HTM Korogwe-Handeni.
Akiwa wilayani Korogwe Waziri Aweso alipokelewa na Mkuu wa Wilaya ya hiyo Jokate Mwegelo kwa Ziara ya kikazi akiwa na lengo la kutatua changamoto mbalimbali na kufuatilia hali ya Utekelezaji wa Miradi ya Maji na hali ya utoaji wa huduma ya Maji eneo la Korogwe mjini.
Pamoja na mambo mengine Waziri Aweso amewaahidi wana Korogwe kuwa Wizara ya Maji inakwenda kusimamia kwa ukaribu kuhakikisha changamoto ya Maji Korogwe inabaki kuwa historia