NA MWANDISHI WETU, NACHINGWEA
MKAZI wa kijiji cha Ngunichile wilaya ya Nachingwea mkoa wa Lindi Mustafa Mkane ( 60 )amepoteza maisha baada ya kushambuliwa na tembo.
Mkane alipoteza maisha kutokana na kundi kubwa la wanyama hao kuvamia mashamba ya wananchi wa Kijiji hicho na vijiji vingine vya kata ya Ngunichile.
Moyo amesema kuwa Aprili 10, 2023 usiku alipokea simu kutoka kwa Ofisa Tarafa ya Lionjo kuwa kuna mwananchi amefariki kutokana na kuvamiwa na tembo hivyo serikali walianza kuchukua hatua ya kuhakikisha wanauzika mwili huo na baada ya ndio wakaenda kukutana na wananchi wa Kijiji cha Ngunichile.
Akithibisha kutokea kwa kifo hicho mkuu wa wilaya ya Nachingwea Mohamed Moyo amesema kifo cha mwananchi wa Kijiji cha Ngunichile kutokana na kuvamiwa na tembo.
Amesema kuwa serikali imechukua hatua ya kuongeza idadi ya askari wa TAWA ili kuwafukuza tembo hao ili wasilete madhara mengine kwa wananchi kama walivyosababisha kifo cha mwananchi huyo.
Moyo amesema kuwa kutokana na kifo hicho na kuharibiwa kwa mashamba ya wananchi wa Kijiji cha Ngunichile serikali ya wilaya ya Nachingwea imetoa tani 20 za chakula kwa ajili ya wananchi ambao wameathirika kutokana na tembo kuvamia mashamba ya wananchi hao.
Kwa upande wake Diwani wa Kata ya Ngunichile Said Makayola ameiomba serikali kutafuta njia ya kudumu kuwaondoa tembo hao katika kata hiyo kutoka na kuleta madhara makubwa kwa wananchi wanaoishi katika Kata hiyo