NA MWANDISHI WETU, HANDENI
MKUU wa Wilaya ya Handeni mkoani Tanga, Albert Msando ameliagiza Jeshi la Polisi wilayani humo, kuwafikisha kwenye vyombo vya kisheria wale wote waliokamatwa kwa kufanya uhalifu katika Kijiji cha Msomera.
Akizungumza wakati akikabidhi gari jipya la polisi kwa ajili ya Kituo cha Polisi Msomera, lililotolewa na Serikali kwa ajili ya jeshi hilo, mkuu huyo wa wilaya amesema hatarajii itokee visingio katika utendaji kazi katika kulinda usalama.
Amewataka polisi waliopangiwa kufanya kazi katika eneo hilo la Msomera kuwa weledi kazini na kutatua changamoto za wananchi kwa wakati.
Kamanda wa Polisi Wilaya ya Handeni, Chimaguli Enock baada ya kukabidhiwa gari hilo, amesema tayari wamewakamata wananchi kadhaa kwa kujihusisha na mambo ya uharifu.
Mkazi wa Msomera, Kwesega Molwe ameshauri Jeshi la Polisi lisisite kuwachukuliwa hatua wale wote watakaobainika kufanya uharifu kijijini hapo.
Serikali imepeleka gari hilo la polisi katika eneo la Msomera kwa ajili ya kuimarisha doria na ulinzi wa mali za wananchi, kutokana na kuibuka wizi hivi karibuni.