NA BENNY MWAIPAJA, WASHINGTON D.C
WAZIRI wa Fedha na Mipango. Dk Mwigulu Nchemba, ameihakikishia Jumuiya ya Kimataifa kwamba Serikali ya Tanzania itaendelea kuwekeza fedha za kutosha kwenye sekta ya kilimo ili kuongeza uzalishaji wa mazao na kuifanya nchi kuwa ghala la chakula duniani.
Dk. Nchemba amesema hayo wakati aliposhiriki, mdahalo wa viongozi wa ngazi ya juu wa nchi za Afrika, kuhusu chakula na kilimo, ulioandaliwa na Taasisi inayojihusisha na uhamasishaji wa masuala ya kilimo Barani Afrika (AGRA), kando ya mikutano ya Kipupwe iliyoandaliwa na Banki ya Dunia (WB) na Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF) ,jijini Washington D.C, Marekani.
Amesema kuwa Serikali imeongeza bajeti ya kilimo kutoka wastani wa shilingi bilioni 250 hadi kufikia shilingi bilioni 950 katika bajeti inayotekelezwa hivi sasa na kwamba mwaka ujao, bajeti hiyo itaongezwa ili kutimiza malengo ya Serikali ya kuifanya sekta hiyo kuwa na tija.
“Mwaka ujao wa fedha tutaongeza tena bajeti hadi kufikia zaidi ya shilingi trilioni moja na kuwekeza kwenye miundombinu ya kilimo ambayo tunaamini itaongeza uzalishaji wa mazao ya chakula na biashara na kuishirikisha sehemu kubwa ya jamii wakiwemo vijana ambao kupitia program ya BBT (Build Better Tomorrow), iliyoasisiwa na Dk.Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, ambayo imelenga kuwakusanya vijana na kuwapatia ujuzi wa masuala ya kilimo” amesema Dk.Nchemba
Naye Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya Kilimo Tanzania, iliyoko chini ya Wizara ya Fedha na Mipango Frank Nyabundege, amesema kuwa Benki yake imewekeza zaidi ya shilingi bilioni 500 katika kuendeleza kilimo nchini Tanzania kwa kuwawezesha wakulima wa kati, wakubwa pamoja na taasisi kadhaa zinazojihusisha na kilimo na kwamba juhudi hizo zitaendelezwa kwa kuwa kilimo ni uti wa mgongo wa Taifa
Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya AGRA, ambaye pia ni Waziri Mkuu Mstaafu wa Ethiopia, Hailemariam Dessalegn, ameisifu Tanzania kwa mikakati inayoichukua ya kuendeleza sekta ya kilimo kwa kuwahusisha vijana na kwamba mpango huo unatakiwa kuigwa na nchi nyingine barani Afrika.
Amesema kuwa usalama wa upatikanaji wa chakula cha kutosha pamoja na usalama wa chakula vinahitaji uwekezaji mkubwa wa rasilimali fedha na kwamba mfano unaotolewa na Tanzania katika kusukuma mbele ajenda ya nchi kujitosheleza kwa chakula ni muhimu na kuahidi kuwa AGRA itaendelea kusaidia juhudi hizo.
Kwa upande wake, Mkuu wa Idara ya Utawala wa Shirika la Kimataifa la Maendeleo la Marekani, Isobel Coleman, amesema kuwa Taasisi yake imejitahidi kuwekeza fedha katika nchi mbalimbali duniani kwa ajili ya kuendeleza kilimo pamoja na usalama wa chakula kwakuwa agenda ya kilimo endelevu na cha uhakika ni muhimu kwa ustawi wa wananchi wakiwemo watoto.
Katika mdahalo huo, nchi za kiafrika ziliombwa kuweka utashi wa kisiasa kwa kuhakikisha kilimo kinapewa kipumbele kwenye mipango yao ya kitaifa kwa kuwekeza kwenye miundombinu ya kilimo cha umwagiliaji kutoka asilimia 10 za sasa hadi kufikia asilimi 50 ifikapo mwaka 2030, utafiti, maafisa ugani, kuwa na masoko ya uhakika, kuwashawishi vijana kushriki shughuli za kilimo, kuongeza mauzo nje ya nchi kutoka dola za Marekani milioni 750 hadi kufikia dola bil. 2/- kwa mwaka, ili kukuza uchumi na maisha ya watu kwa ujumla.