NA MWANDISHI WETU, DAR ES SALAAM
CHAMA cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kimemtaka Rais kuchukua hatua zaidi dhidi ya viongozi wanaodaiwa kuhusika na ubadhirifu wa fedha za umma na matumizi mabaya ya ofisi katika ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG).
Katibu Mkuu wa Chadema, John Mnyika amesema leo Aprili 10 wakati akitoa taarifa ya uchambuzi wa ripoti za CAG kuwa uamuzi wa Rais Samia Suluhu Hassan kuvunja bodi ya Shirika la Reli Tanzania (TRC) na kutengua uteuzi wa Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Ndege za Serikali hautoshi.
“Rais ana Mamlaka makubwa kikatiba, bado Rais hajatumia Mamlaka yake makubwa ya kikatiba ya kutosha kuchukua hatua juu ya waliobainika kufuja mali za umma na kusababisha hasara kwa Serikali,” Myinka amesema katika taarifa yake kwa waandishi wa habari jijini Dar es Salaam.
“Kuvunja Bodi ya TRC na kutengua uteuzi wa Mtendaji Mkuu wa TGFA (Mhandisi John Nzulule) pekee haitoshi bali hatua zaidi zinapaswa kuchukuliwa.”
“Lazima tutazame mchakato wa ununuzi wa Ndege hizi na pia hasara ya uendeshaji wa ATCL,” ameongeza Mnyika.
Hata hivyo, Mnyika amehoji ikiwa maamuzi ya Ikulu kuvunja Bodi ya TRC inamaanisha pia, Rais ametengua uteuzi wa Mtendaji Mkuu wa Shirika hilo, Masanja Kadogosa.
Ripoti ya ukaguzi ya CAG imeonesha kuwa TRC ilimkataa Mzabuni aliyetaka kulipwa Sh bilioni 616.4 na kumpa kazi Mzabuni wa Sh trilioni 1.119 sawa na ongezeko la Sh bilioni 503.2 (asilimia 82) isiyokuwa na ulazima
Pia, katika ununuzi wa ‘Locomotives’ na Makochi ya Abiria, Shirika la Reli (TRC) lilitekeleza Mkataba bila dhamana ya Utendaji na kusababisha hasara ya Sh bilioni 13.7 kutokana na Mkandarasi kushindwa kutimiza Masharti ya Mkataba
Akichambua ripoti hiyo, Mnyika amesema hasara hiyo ina mnyororo mrefu, “sio Bodi ya TRC pekee yake,” akisisitiza kuwa mchakato wa kuingia mkataba wa malipo yaliyohusu Mzabuni huyu hayakuihusu Bodi pekee yake.
“Mchakato ulihusu Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali lakini taarifa tulizonazo ni kwamba idhini ya kufanya malipo ilifanywa na Wizara ya Fedha kwa barua ya Katibu Mkuu wa Hazina aliyekuwepo wakati huo Dotto James lakini vilevile kwa idhini ya Waziri wa Fedha aliyekuwepo wakati huo.”alihitimisha Mnyika