ELDORET, KENYA
MAHAKAMA ya Eldoret nchini Kenya imemtia hatiani mwanaume mmoja aliyefahamika kwa jina la Humphrey Shilisia kwa kumuhukumu adhabu ya miaka 210 kutokana na makosa mbalimbali.
Mwanamume huyo mwenye umri wa miaka 55 aliyeshtakiwa kwa makosa manne ya wizi wa kimabavu na shtaka jingine la ubakaji nchini Kenya.
Hakimu Mkuu wa Eldoret, Naomi Wairimu amesema upande wa mashtaka umethibitisha kesi yake bila shaka yoyote.
Shilisia alifikishwa mahakamani kwa wizi wa kimabavu pamoja na mkewe Amina Melesi na mtuhumiwa wa tatu, David Gazemba.
Hakimu Wairimu aliwaachia Melesi na Gazemba kwa msingi kwamba hakukuwa na ushahidi wa kutosha kuwatia hatiani kutokana na mashtaka yaliyokuwa yanawakabili.
Katika kila mojawapo ya makosa manne ya uhalifu huo, Wairimu alimhukumu Shilisia miaka 50 jela.
Mshtakiwa huyo pia alipatikana na hatia ya ubakaji na alihukumiwa kifungo cha miaka 10 jela kwa kosa hilo, huku hukumu zote mbili zikitakiwa kwenda sambamba.
Kwa mujibu wa maelezo ya mwendesha mashtaka, Shilisia ameshtakiwa kwa kuiba Sh.6,000 za Kenya (sawa na Sh.107,169 za Kitanzania) kwa akiwa amejihami kwa silaha butu katika eneo la Wales Estate, Kapseret Juni 20, 2020.
Shilisia anakabiliwa na shtaka la pili ambapo alishtakiwa kwa kumwibia Yulita Mitei, sh. 19,300 za Kenya (sawa na Sh 344,727 za Tanzania). Walikabiliwa na shtaka la tatu na la nne la kuwaibia Moses Rotich na Gilbert Murei KSh 76,800 (sawa na Sh137,1764 za Kitanzania) ( na KSh 4,800 (sawa na Sh8,5735 za Kitanzania).
Shahidi muhimu katika shtaka la kwanza, alieleza siku ambayo mshtakiwa alivamia nyumba yao akiwa amebeba tochi ya kuwamulika machoni kisha kumnyang’anya simu na kujitumia sh. 6,000 za Kenya (107,169) kwenye simu yake.
“Kisha alihamisha fedha kutoka kwenye simu ya mume wangu na kumwamuru aingie chini ya kitanda na kuniburuta nje ya nyumba akiwa ameniwekea panga shingoni ambapo alinibaka,” shahidi huyo ameileza mahakama.
Taarifa za kitabibu zilizowasilishwa mahakamani hapo zilionesha kuwa Shilisia alimwingilia kinguvu mwathiriwa.
Shilisia katika utetezi wake aliwashutumu maofisa wa polisi akisema wamembambikia makosa akidai walimkamata wakati alipokuwa anakwenda kazini.