NA MWANDISHI WETU, DAR ES SALAAM
VYAMA viwili vya upinzani nchini Tanzania vya Chadema na ACT Wazalendo, kesho Jumatatu, Aprili 10, 2023 vinatarajia kufanya mikutano na waandishi wa habari kuchambua ripoti ya Mkaguzi na Mdhibiti wa Hesabu za Serikali (CAG).
Wakati Chadema kinatarajia kuanza uchambuzi wake mbele ya wanahabari saa 3.30 asubuhi, ACT Wazalendo wataanza Saa 5.00 asubuhi.
Uchambuzi wa ACT Wazalendo utakaofanywa na kiongozi wa chama, Zitto Kabwe utafanyika kwenye ukumbi wa moja ya hoteli zilizopo Dar es Salaam ilhali uchambuzi wa Chadema utafanywa na Katibu Mkuu wa chama hicho, John Mnyika kwenye makao makuu ya chama yaliyopo Kinondoni jijini Dar es Salaam.
Tayari mgongano wa chambuzi hizo zinazofanywa siku moja umezua mijadala kwenye mitandao ya jamii huku wanachama kutoka kwenye vyama hivyo wakirushiana vijembe.
Wanachama wa ACT Wazalendo wameonekana wakijinasibu kuwa wao ndio walikuwa wa kwanza kutangaza kufanya uchambuzi huo huku wale wa Chadema wakisema kila chama kina haki ya kufanya jambo lake na kulitangaza kwa muda wanaodhani ni muafaka.