NA MWANDISHI WETU, DAR ES SALAAM
KAMPUNI ya simu za mkononi ya Airtel Tanzania imeandaa hafla ya futari Kwa wafanyakazi wake waislamu na wakristo ikiwa ni ishara ya shukurani na pia kudumisha umoja na mshikamano baina ya wafanyakazi hao.
Akizungumza wakati wa hafla hiyo Aprili 6, 2023 Mkurugenzi Mtendaji wa Airtel Dinesh Balsingh amesema hafla hiyo imekuwa ya baraka mno ukizingatia kuwa kipindi hiki waislamu kote nchini wanaendelea na mfungo wa mwezi mtukufu wa Ramadhani hali kadhakika waumini wa dini ya kikristo wao wakimaliza mfungo wao wa Kwaresma.
“Sisi kama Airtel Tanzania tunaamini mshikamano mahali pa kazi ndio siri kubwa ya mafanikio yetu, hivyo hafla kama hizi ni muhimu sana katika kuendelea kuwaweka wafanyakazi pamoja na kudumisha moyo wa upendo, umoja na mshikamano miongoni mwao”
“Kwa namna ya kipekee tungependa kuwashukuru wafanyakazi wote wa Airtel kutoka katika Kila idara, wafanyakazi wa kada zote kwa jitihada zao bila kuchoka katika kuwahudumia wateja wetu, wao ndio siri ya ubora wa mtandao na huduma zetu bora, ni matumaini yetu kuwa jitihada hizo na uchapakazi wao utaendelea kuiweka Airtel Tanzania kileleni linapokuja suala la huduma bora za simu za mkononi nchini”, amesema Balsingh
Aidha Balsingh amesema Airtel Tanzania inawatakia wafanyakazi wake wote pamoja na wateja wake heri ya msimu wa sikukuu za Pasaka zinazoanza kuadhimishwa na wakristo wote duniani kuanzia leo Aprili 7 hadi Jumatatu Aprili 10 huku ikiendelea kuwatakia mfungo mwema wa Ramadhani waumini wa dini ya kiislamu.
“Pamoja na hayo tunawatakia watanzania wote Sikukuu njema ya Pasaka na mfungo mwema wa Ramadhani huku mkiendelea kufurahia mtanda bora kila mahali, bidhaa na huduma zetu bora za mtandao wetu wenye nguvu pamoja na ofa lukuki, vifurushi kabambe bila kusahau zawadi bomba zinazotolewa kupitia kampeni zetu mbalimbali zinazoendelea” amehitimisha Mkurugenzi huyo wa Airtel