NA JANETH JOVIN, DAR ES SALAAM
BARAZA la Taifa la Mashirika Yasiyo ya Kiserikali (NACoNGO), limeanza kuzihoji NGO 29 zilizotuhumiwa na aliyekuwa Waziri wa Sheria na Katiba, Dk. Harrison Mwakyembe dhidi ya tuhuma za uwepo wa shughuli za vitendo vya ushoga (LGBTQ) nchini zilizoibuliwa hivi karibuni na waziri huyo wa zamani.
Akizungumza na waandishi wa habari Jijini Dar es Salaam leo Aprili 2, 2023 Mwenyekiti wa NACoNGO, Dk. Lilian Badi, amesema Kamati tendaji kwa kushirikiana na Kamati ndogo ya maadili ya baraza hilo, imeanza kumuhoji Waziri huyo wa zamani juu ya utafiti wake aliyofanya hivi karibuni uliotaja mashirika yanayofanya shughuli hizo.
Dk. Badi amesema, Dk. Mwakyembe atahojiwa ili kueleza kinagaubaga kuhusu utafiti wake huo uliobaini uwepo wa baadhi ya NGO zinazohamasisha vitendo vya ushoga nchini, kinyume cha sheria na maadili.
“Tumefanya kikao cha dharura cha Kamati tendaji ilikujadili, kuchanganua hali na kuweka maazimio ya utekelezaji kuhusiana na suala hili,hata hivyo kumefanyika mawasiliano ya awali na mashirika yote yaliyohusishwa ikiwa ni maandalizi ya kuwafanya uchunguzi na mahojiano ya kina, kamati yetu inaandaa namna bora yakufanya zoezi la uchunguzi,” amesema na kuongeza kuwa
“Tumeomba kukutana na kamati ya Dk. Mwakyembe ilitupate taarifa yao na pia tuwaeleze maoni yetu na Juhudi tunazozichukua kama viongozi wa sekta ya NGO’s baada ya kukamilisha hayo tutaandaa taarifa yetu pamoja na kutoa tamko kwa umma kwa watanzania hususani wadau na wabia wa shughuli za NGO’s nchini,”amefafanua
Aidha amesema Dk. Mwakyembe atawaeleza alifanyaje tafiti, amegundua nini na kwa nini aliamua kutoa taarifa hiyo hivyo anatoa maelezo yake na yakikamilika NACoNGO itatoa taarifa kwa umma.
Amesema baada ya kamati hizo kumaliza kuwahoji wahusika wote hatua za kisheria zitachukuliwa kwa mashirika yatakayobainika kuhusika na vitendo hivyo.
Mwenyekiti huyo wa NACoNGO, alitaka sekta ya mashirika yasiyo ya kiserikali kuwa watulivu katika kipindi ambacho baraza hilo linafanyia kazi tuhuma zinazoibuliwa.
“Kama NACoNGO tunataka kuilinda jamii yetu na kubaki salama katika suala hili lililokinyume na maadili ni vyema kuungana kuwa pamoja kuliko kunyoosheana vidole,hivyo wanasekta ya NGOs tuepuke kuhukumu baadhi ya makundi ama taasisi hadi hapotutakapokuwa na taarifa kamili na kudhibitika bila mashaka kuwa watu fulani au makundi fulani wamehusika,”amesema Dk. Badi.
Hata hivyo amesema mijadala kuhusu suala hilo ingoje taarifa rasmi ya NaCoNGO kuhusu hali halisi itakayotia ndani uchunguzi kwa mashirika yote yaliyohusishwa na tuhuma hizo,na pia taarifa yao itafikishwa katika bodi ya uratibu ya NGO’s kupitia Ofisi ya msajili wa NGO’s Tanzania Bara.