NA MWANDISHI WETU, DAR ES SALAAM
CHUO Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) Ndaki ya Sayansi ya Jamii kimeiomba Serikali kuhakikisha faida zinazotokana na ushirikiano katika kuhifadhi maliasili nchini zinagawanywa kwa usawa kwa wanajamii na kuepuka kufaidisha watu wachache.
Hayo yalibainishwa jijini Dar es Salaam leo Aprili 2, 2023 na Rasi wa Ndaki ya Sayansi ya Jamii UDSM, Profesa Christine Noe wakati akizungumza na waandishi wa habari juu ya mapendekezo yaliyotolewa katika kitabu cha Hoja Kinzani kwenye uhifadhi maliasili kinachotarajiwa kuzinduliwa Aprili 4, mwaka huu.
Prof. Noe amesema ongezeko la ushirikiano katika shughuli za kuhifadhi maliasili umeleta matokeo chanya katika sekta ya misitu, nchi kavu na habarini hivyo ni muhimu kwa jamii iliyozunguka maeneo yaliyohifadhiwa hifadhiwa zikapata faida kwa usawa ili kuepuka kuwanufaisha wachache.
“Ni muhimu pia kwa Serikali kumaliza mgongano au kutokueleweka kwa mgawanyo wa majukumu ya wadau mbalimbali wa uhifadhi unaopunguza ufanisi wa malengo ya ushirikiano, lakini kuwepo na malengo ya muda mrefu ya upatikanaji endelevu wa fedha za kugaramia shughuli za uhifadhi,” amesema na kuongeza
“Hata hivyo serikali inapaswa kuhakikisha kwamba juhudi za kuwashirikisha wananchi zinawenda sambamba na kujenga imani kwamba jamii hizo ni wamiliki wa maliasili na kwamba wanaweza kuiamini serikali na wadau wengine, vinginevyo bado kuna mashaka makubwa kama wanajamii ni wadau wanufaika,” amesema Prof. Noe
Aidha Noe amesema mabadiliko ya hali ya maisha ya jamii za vijijini yanapatikana pale tu ambapo uzalishaji kwenye kilimo umeongezeka na masoko yanapatikana, kwamba hiyo inamaanisha kwamba japo ushirikishwaji katika shughuli za uhifadhi umeleta ubora wa sera na kufungua fursa za biashara.
Amesema licha ya juhudi hizo bado uhifadhi haujaweza kuwa tegemeo katika kuleta maendeleo kwa jamii hasa zile za wakulima kwani ilitegemewa kwamba ushirikishwaji wa jamii katika uhifadhi kungesababisha pia madaraka ya kufanya maamuzi mbalimbali kuhusu maliasili.
“Kitabu hiki cha Hoja Kinzani kitakachozinduliwa Aprili 4, 2023 ni hitimisho la mradi wa miaka mitano wa ushirikiano mpya katika uhifadhi na maendeleo ya kiikolojia na jamii kimetoa mapendekezo ya kisera ambapo kama yatafanyiwa kazi na serikali tutaweza kuinua sekta ya misitu, bahari na nchi kavu,” amesema
Naye Mtaalamu wa Uvivu na Usimamizi wa Mazingira ya Pwani na Barani Ndaki ya Sayansi ya kilimo na teknolojia ya chakula (USDM), Dk. Robert Katikilo amesema tunapoelekea kwenye uchumi wa buluu tuna kila nafasi ya kuona na kuhakikisha uhifadhi ya maliasili unaimarika.
Dk. Katikilo ambaye ni Mhadhiri Mwandamizi UDSM, amesema ni dhahiri kwamba ongezeko la wadau na washiriki katika uhifadhi wa maliasili umelenga kwenye kutafuta maendeleo endelevu katika uhifadhi na jamii zinazozunguka maeneo yaliyohifadhiwa.