NA MWANDISHI WETU, DAR ES SALAAM
NDUGU wa Majeruhi aliyegongwa na basi la Mwendokasi februari 22, 2023 eneo la Kisutu jijini Dar es salaam , Osam Milanzi (38), Shaaban Milanzi amesema ndugu yake anahitaji msaada zaidi ili kuiwezesha familia yake kujikimu kimaisha.
Miongoni mwa msaada anaohitaji Osam ni pamoja na vyakula,matibabu zaidi na ada za watoto wake watatu ambao wanasoma.
Shaaban aliyasema hayo jana Aprili 1, 2023 alipofanya mahojiano maalum na Demokrasia .
Alisema tangu Osam alipopata ajali familia yake imeyumba na wakati mwingine hulazimika kukopa au kusaidiwa ili kukidhi mahitaji ya familia .
“Osam alikuwa ndio kila kitu katika familia hivyo ajali aliyoipata imeipa familia ugumu wa maisha kiasi kwamba binti yake wa kwanza Ibtisam Osam mwanafunzi wa kidato cha tatu shule ya sekondari Manzese amekwama kimasomo” alisisitiza
Aidha alieleza kuwa mbali ya binti yake wa kwanza , lakini pia Osam ni baba wa watoto watatu huku mtoto wa pili ni mwanafunzi wa shule msingi na wa mwisho yupo elimu ya awali ambao wote wanahitaji kulipiwa ada ili waendelee na masomo.
Wakati huo huo Shaabani aliiambia Demokrasia kuwa Osam anahitaji msaada wa haraka kwani hata nyumba anayoishi ni ya familia na maisha ni magumu tangu apate ajali mambo mengi yamesimama.
Alibainisha kuwa anawaomba watanzania wamsaidie kaka yake katika kipindi hiki kigumu.
Kuhusu utaratibu wa fidia ya kaka yake, alisema anaishukuru serikali kupitia UDART kuisaidia familia kwenye upande wa matibabu kipindi ambacho Osam akiwa MOI akiendelea na matibabu.
Alisema kwasasa familia haipo tayari kuzungumzia suala la fidia hadi pale Osam atakapotengamaa kwani mfuatiliaji wa stahiki zake ni yeye mwenyewe.
“Wakati ajali ilipotokea mimi binafsi nilikwenda Polisi na UDART ambapo nilielezwa utaratibu wa kisheria unaotakiwa kufuatwa hivyo nilielewa na kama familia tumeliacha hadi pale kaka yangu(Osam) atakapoimarika kiafya” alihitimisha