NAIROBI, KENYA
JESHI la Polisi katika eneo la Narok ya kusini wamemtia mbaroni mzee wa miaka 60 kwa kosa la kutowapeleka shuleni jumla ya watoto wake 20.
Kwa mujibu wa Naibu Kamishna wa kaunti hiyo Felix Kisalu, mzee huyo amekuwa akipinga vikali kuwasomesha watoto wake licha ya kutajwa kuwa na uwezo wa kufanya hivyo.
Mzee huyo hajawahi kumchukua hata mmoja wa watoto wake 20 kutoka kwa wake tofauti shuleni licha ya kushinikizwa kufanya hivyo kwa muda mrefu.
Kwa mujibu wa ripoti, hakuna mtoto wake hata mmoja ambaye amechukuliwa kupitia mfumo wa elimu hadi kukamilishwa huku wengi wao wakikatisha elimu ya shule ya msingi.
“Licha ya kuwa na mali ya kutosha kusaidia na kusomesha watoto wake, wengi wao wamelazimika kuacha shule,” amesema Kisalu.
Wakati huo huo imeelezwa kuwa mzee huyo yupo taabani kwa vile inasemekana alikodisha zaidi ya ekari 100 za ardhi na kupata mapato ya kutosha lakini “anachagua kupuuza familia yake na kufuja pesa za kukodisha katika soko la Ololunga kila siku”.
Alikamatwa na kushililiwa katika Kituo cha Polisi cha Ololulunga na atafikishwa kortini na Idara ya watoto.
Kisalu ameghairi ukodishaji wa ardhi yake na kumtaka yeyote atakayeikodisha kupeleka pesa hizo moja kwa moja kwa shule za watoto wa mzee huyo.
Zaidi ya hayo, msimamizi huyo sasa ameapa kupiga mnada mifugo ya wazazi ambao hawakuwa wanawasomesha watoto wao huku Kaunti Ndogo ikielekea kwenye mpito wa asilimia 100.