NA MAGENDELA HAMISI, DAR ES SALAAM
WAWAKILISHI pekee wa Tanzania katika michuano ya Kombe la Shirisho Afrika (CAFCC), Yanga imefanikiwa kuendeleza rekodi ya kushinda katika uwanja wa Benjamin Mkapa na kujiweka salama katika hekaheka ya kutinga hatua ya robo fainali ya mashindano hiyo baada ya kushinda kwa mabao 2-0.
Kikosi hicho kinachonolewa na Kocha Mohamed Nabi katika mchezo wa leo, imefanikiwa kuitwanga Real Bamako ya Mali katika mchezo wa marudiano ambapo katika mtanange wa uliochezwa ugenini timu hizo zilitoka sare ya bao 1-1.
Katika mchezo wa leo, Fiston Mayele ameendelea kuwa mwiba kwa Real Bamako baada ya kufanikwa kufunga bao la kwanza dakika ya nane kipindi cha kwanza huku dakika 54 aliangushwa katika eneo la miguu 18 akiwa anakwenda kumsabahi mlinda mlango.
Yannick Bangala ambaye alipewa jukumu la kupigwa mkwaju huo wa penati, kwa mashangao wa watazamaji waliofika katika dimba hilo la Mkapa alipaisha pigo na kuikosesha Yanga kuandika bao la pili katika mtanange huo.
Dakika ya 67, Yanga waliandika bao la pili kupitia kwa Juses Moloko baada ya kupora mpira kwa washambuliaji wa Bamako waliokuwa wakishambulia na kuukokota na kufanikiwa kuwatambuka mabeki na kuachia shuti lilija wavuni.
Hadi kipyenga cha mwisho kinapulizwa Yanga wakaondoka na ushindi wa mabao 2-0 na kujiweka katika nafasi ya pili katika msimamo wa kundi D ikiwa na alama saba mkononi na wakiongozwa na Monastri ya Tunisia yenye alama 10 kibindoni na kuwa timu ya kwanza kutinga hatua ya robo fainali ya michuano hiyo.
Timu ya Monastri imekuwa ya kwanza kutinga robo fainali baada ya kufanikiwa kuitwanga TP Mazembe ya DRC kwa bao 1-0 na kufikisha alama 10 ambazo zinaweza kufikiwa na Yanga pekee ikiwa itashinda mchezo ujao.
Na katika mchezo ujao utaokapigwa Machi 18 , 2023 kwenye dimba la Mkapa, Yanga watawakaribisha Monastri ya Tunisia.