NA MWANDISHI WETU, DAR ES SALAAM
WAZIRI wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Nape Nnauye anatarajiwa kuwa mgeni rasmi katika kongamano maalum lenye lengo la kujadili kwa kina maendeleo ya teknolojia na athari zake hasa kwa wanawake.
Kongamano hilo ambalo litafanyika Machi 7, 2023 jijini Dar es Salaam katika Ukumbi wa Mikutano wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNICC) linatarajiwa kuwaleta pamoja wataalamu wakuu, na watu tofauti tofauti kutoka sekta mbalimbali ili kujadili pia namna ya kuwawezesha wanawake na kuongeza ushiriki wao katika tasnia ya teknolojia.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam, Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika lisilo la faida la The LaunchPad Tanzania ambao ndio waandaaji wa kongamano hilo, Carol Ndosi amesema kwa kasi ya maendeleo ya kiteknolojia iliyopo sasa ni muhimu wanawake kukutana na kujadili namna ambavyo watapewa fursa sawa za kuchangia na kuunda mustakabali wa teknolojia.
Amesema wanaamini kwamba ushirikishwaji wa wanawake katika teknolojia ni muhimu kwasababu kundi hilo huleta mtazamo wa kipekee kwenye meza kuu za majadiliano.
“Mkutano huu utatoa jukwaa kwa wanawake kuonyesha kazi zao, kubadilishana uzoefu wao, na kuungana na wengine katika tasnia hii, tunajivunia kuwa na safu bora ya wazungumzaji wakuu, wanajopo ambao watatoa mada mbalimbali, ikiwa ni pamoja na ukuaji wa teknolojia kama fursa kwa wanawake, teknolojia na ubunifu wa kujumuisha usawa wa jinsia,” amesema Ndosi
Aidha Ndosi amesisitiza kuwa kongamano hilo ni la wazi kwa mtu yeyote anayevutiwa na teknolojia na jukumu la wanawake katika kuunda mustakabali wake kuweza kushiriki na kwamba wanaamini kwamba kwa kuleta pamoja watu tofauti, wanaweza kukuza mijadala yenye maana na kuleta mabadiliko chanya.
“Tunamwalika kila mtu kujiunga nasi katika shughuli hii muhimu na kuwa mfadhili wa kongamano hili la wanawake na tknolojia. Hebu tushirikiane kuwawezesha wanawake na kuendeleza maendeleo katika tasnia ya teknolojia,” amesema Ndosi.