NA MWANDISHI WETU, DAR ES SALAAM
UKAGUZI wa Bomba la Kusafirisha Gesi Asilia kutoka katika kisima cha MB1 hadi ulipo mtambo wa kuchakata gesi hiyo uliopo Mnazi Bay, Mtwara, unatarajiwa kuanza hivi karibuni.
Akizungumza jijini Dar es Salaam, Meneja Mkuu wa kampuni ya Maurel and Prom Exploration Tanzania Limited (M&P), Nicolas Engel amesema ukaguzi huo unaanza baada ya kampuni yake kusaini mkataba maalum na kampuni ya kitanzania ya Solution Tag Consulting Company Limited.
Engel amesema mkataba huo utahusisha kukagua na kusafisha bomba la gesi asili lenye urefu wa mita 800 kutoka kwenye kisima inapozalishwa hadi ulipo mtambo wa kuchakata gesi hiyo.
“Kazi hii pia itahusisha kukagua na kusafisha bomba la kilometa 27 linalosafirisha gesi kutoka ulipo mtambo wa kuchakata gesi uliopo Mnazi Bay hadi kilipo kituo cha kupokea gesi asilia cha M&P kilichopo Mtwara Mjini,” amesema.
Engel amesema kutiwa saini kwa mkataba huo wenye thamani ya zaidi ya Sh. bilioni moja za Kitanzania ni hatua kubwa katika kuhamasisha na kuwezesha Watanzania kushiriki katika shughuli za mafuta na gesi asilia nchini, kwani awali kazi hizo za kitaalamu zilikuwa zikifanywa na kampuni za nje ya nchi.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa kampuni ya Solution Tag Consulting Company Limited, Peter Kichogo amesema mkataba huo utawapa fursa ya kuonesha uwezo wa kampuni za Kitanzania katika shughuli hizo na kuondoa dhana ya kutegemea kampuni kutoka nje.
“Kwa kipindi kirefu huduma hizi za kitaalamu zimekuwa zikitoka nje, hivyo hii ni fursa kwetu kuonesha uwezo wa kampuni za ndani.”
“Kwa hatua hii, ni ishara kuwa wawekezaji katika sekta ya mafuta na gesi wako tayari kutuamini Watanzania na tutatumia wataalamu wa Kitanzania kukamilisha hili,” amesema.
Charles Nyagi wa Mamlaka ya Udhibiti Mkondo wa Juu wa Petroli (PURA)…. amesema hatua hiyo ni mwanzo mzuri kwa kuwa miaka ya nyuma fursa hizo hazikuwepo kwa Watanzania, hivyo ni matokeo mazuri ya Serikali kuweka kanuni zinazowaelekeza wawekezaji kwenye sekta hiyo kutoa kazi hizo kwa kampuni za Kitanzania.
Nyangi ambaye ni Mkuu wa Kitengo cha Ushirikishwaji wa Wazawa na Uhusishwaji wa Wadau wa PURA amesema kwa hatua hiyo wanatarajia mafanikio zaidi na kufungua milango kwa kampuni nyingine za Kitanzania kufuatilia na kupata fursa hiyo kupitia PURA.
“PURA itaendelea kuhakikisha Watanzania na kampuni za Kitanzania zinapewa kipaumbele wakati wa utekelezaji wa shughuli za mkondo wa juu wa petroli,” amesema.
Ameeleza kuwa hiyo ni sehemu muhimu ya usimamizi bora wa matakwa ya Sheria ya Petroli ya mwaka 2015, kuhusu ushiriki wa Watanzania katika shughuli za mkondo wa juu wa petroli zinazojumuisha utafutaji, uendelezaji na uzalishaji wa mafuta na gesi asilia nchini.
Amesema kwa mujibu wa sheria, manunuzi ya bidhaa na huduma katika shughuli za mkondo wa juu wa petroli inapaswa yafanyike ndani ya nchi na kufanywa na kampuni za kizawa.
Ameongeza kuwa pale ambapo huduma inayohitajika na kampuni za utafutaji wa mafuta na gesi haipatikani nchini, PURA imekuwa ikihakikisha kampuni kutoka nje inayoshinda zabuni inaingia ubia na kampuni za Kitanzania kwa lengo la kuwajengea uwezo.
Ends