NA MWANDISHI WETU, DAR ES SALAAM
MAWAKILI wanaokiwakilisha Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) wamesitisha kuwahoji mashahidi ambao ni wabunge 19 waliofungua mashitaka mahakama kuu wakipinga kuvuliwa uanachama wa chama hicho.
Kesi hiyo iliyoendelea leo Jumatatu, Machi 06, 2023 baada ya kuahirishwa Desemba mwaka jana ilitarajiwa mawakili wa Chadema wakiongozwa na Peter Kibatala waendelee kumhoji Jesca Kishoa kisha Ester Matiko, Ester Bulaya na baadae Halima Mdee.
Lakini mawakili wa Chadema baada ya kushauriana waliamua kuachana kuendelea kuwahoji mashahidi hao ambao ni wabunge wa viti maalumu wanaotambulika kama hawana chama baada ya kuvuliwa uanachama.
Demokrasia lilimpata mmoja wa mawakili wa Chadema, Hekima Mwasipu ambaye alithibitisha taarifa hizo. Alipoulizwa kwanini walifikia maamuzi hayo, Mwasipu alisema upande wao umeridhika na ushahidi waliokwishakuupata walipowahoji baadhi ya wabunge hao ushahidi ambao utaisaidia mahakama kuu kutoa hukumu ya kesi hiyo..
Kitendo hicho kimepelekea Mawakili wa akina Mdee kuiomba mahakama kuu iwaite mahakamani hapo wajumbe wa bodi ya wadhamini wa chama hicho ombi ambalo lilikubaliwa.
Akizungumza na Demokrasia , mmoja wa mawakili wa wabunge hao, Edson Kilatu amesema Machi 09 kesi hiyo itaendelea na wataanza kumuhoji Ezaveli Lwaitama na baadae Ruth Mollel ambao ni wajumbe wa bodi ya wadhamini wa Chadema.
Wabunge hao 19 wakiongozwa na Halima Mdee walifungua kesi wakipinga kuvuliwa uanachama na Kamati Kuu ya chama hicho. Wabunge hao walikata rufaa kwenye baraza kuu la chama hicho lakini Mei 11, 2022 rufaa yao ilitupiliwa mbali.
Iliwalazimu wabunge hao kukimbilia mahakama kuu wakipinga kuvuliwa uanachama hali iliyopelekea wasifukuzwe bungeni mpaka kesi yao itakapokamilika.
Leo Jumatatu, Machi 06 kwenye mtandao wa Clubhouse, Spika wa Bunge la Tanzania, Tulia Ackson alisema punge lake linasubiri uamuzi ya mahakama.
“Sisi hatuwezi kufanya chochote, mpaka mahakama kuu itakapotoa hukumu ya kesi hiyo. Kama mahakama ikiridhia wabunge hao kufutwa uanachama basi na sisi tutawaondoa Bungeni,” amesema Dk Tulia.
Wabunge hao 19 ni Halima Mdee, Esther Matiko, Grace Tendega, Cecilia Pareso, Ester Bulaya, Agnester Lambart, Nusrat Hanje, Jesca Kishoa, Hawa Mwaifunga, Tunza Malapo, Asia Mohammed, Felister Njau na Naghenjwa Kaboyoka.
Wengine ni Sophia Mwakagenda, Kunti Majala, Stella Flao, Anatropia Theonest, Salome Makamba na Conchesta Rwamlaza.