NA MWANDISHI WETU, ARUSHA
RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan anatarajiwa kuwa mgeni rasmi kwenye kongamano la Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) lililoandaliwa na Baraza la Wanawake (Bawacha) wa chama hicho.
Akizungumza na vyombo vya habari leo Jumapili, Machi 05, Mwenyekiti wa Chadema Taifa, Freeman Mbowe, amesema Rais Samia amethibitisha kuwa mgeni rasmi kwenye kongamano hilo litakalofanyika Machi 08 Moshi mkoani Kilimanjaro.
“Kongamano hili la siku ya wanawake duniani ni la wanawake wote, lakini hapa Tanzania, Bawacha wamekuwa wakiliandaa kwa mafanikio makubwa kila mwaka na wamekuwa wakitoa hotuba zenye jumbe mbalimbali zinazowahusu wanawake wote bila kujali itikadi za vyama vyao.
“Napenda kuwatangazia kuwa Rais Samia ambaye nilikuwa na mazungumzo naye jana Jumamosi, amekubali kuwa mgeni Rasmi siku hiyo na mimi nitampokea mjini Moshi siku hiyo,” amesema Mbowe
Rais Samia kukubali kuhudhuria na kuwa mgeni rasmi kwenye kongamano linaloandaliwa na chama kikuu cha upinzani ni matunda ya maridhiano ya kisiasa yanayoendelea kufanywa na chama chake (CCM) na Chadema.
Maridhiano hayo awali yalianza baada ya Rais Samia kuunda kikosi kazi cha kuishauri serikali kuhusu mwenendo wa kisiasa nchini.
Lakini maridhiano yalitiwa chachu baada ya kikao cha kwanza kati ya Rais Samia na Mbowe kukutana Ikulu, Machi 04, 2022 siku ambayo Mbowe alitoka gerezani baada ya Serikali kuifuta kesi ya ugaidi iliyokuwa inamkabili mwanasiasa huyo.
Kati ya mambo ambayo Chadema waliyapeleka kwa Rais na kutaka yarekebishwe haraka ni pamoja na kuwaachia huru wafungwa wa kisiasa wa Chadema, jambo ambalo kwa asilimia kubwa limeshafanyika.
Jambo la pili ni kuweka usalama kwa wakimbizi wa kisiasa waliokimbia nchi. Tayari viongozi wa Chadema waliokimbia nchi wamesharejea. Viongozi hao ni Tundu Lissu, Ezekia Wenje na Godbles Lema.
Jambo la tatu lililodaiwa na Chadema ni kuondoa zuio la mikutano ya hadhara ambapo tayari Januari mwaka huu, Rais Samia ameondoa zuio hilo.
Jambo la nne ni upatikanaji wa Katiba mpya ambapo mpaka sasa mchakato haujaanza.