NA MWANDISHI WETU, DAR ES SALAAM
CHAMA cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kimeanza kupokea ruzuku waliogoma kuichukua baada ya uchaguzi mkuu wa Oktoba 2020.
Uthibitisho huo umetolewa na Makamu Mwenyekiti wa chama hicho, Tundu Lissu leo Jumapili, Machi 05, 2023 wakati akijibu maswali kwenye hadhara iliyofanyika kwenye mtandao wa Clubhouse.
“Chama (Chadema) kimeanza kupokea ruzuku mwezi huu (Machi) ambayo hatukuichukua tangu ulipofanyika uchaguzi mkuu wa 2020.
“Tumepokea sehemu tu ya pesa hizo na kiasi kilichosalia tutapewa siku za usoni. Tumeamua kuichukua kwasababu ya ahadi ya maridhiano yanayoendelea,” alisema Lissu
Hata hivyo mwanasiasa huyo alisema hivi karibuni Katibu Mkuu wa chama hicho, John Mnyika au Mwenyekiti, Freeman Mbowe atatoa taarifa rasmi.
Chadema iligoma kuchukua ruzuku hiyo inayokadiriwa kuwa ni zaidi ya sh. Milioni 110 baada ya kukataa matokeo ya uchaguzi waliyodai haukuwa uchaguzi bali ulikuwa ni uchafuzi.
Kwenye kauli za chama hicho walisikika wakisema kuwa wanaukataa uchaguzi na mazao yake.
Ikumbukwe chama hicho pia kilikataa kupeleka wabunge wa viti maalum bungeni kwa sababu ya kutoutambua uchaguzi huo.
Hii ni hatua nyingine ya matunda ya maridhiano yanayoendelea baina ya chama hicho na serikali.