NA MAGENDELA HAMISI
TIMU za Mtibwa Sugar ya Manungu mkoani Morogoro na Ihefu ya jijini Mbeya zimeungana na Simba na Yanga kwenye hatua ya Robo Fainali ya michuano ya Kombe la Shirikisho la Soka la Tanzania ‘ Azam Sports Federation Cup’ (ASFC).
Mtibwa Sugar katika mchezo wa leo uliopigwa kwenye dimba la Jamhuri, Morogoro ilifanikiwa kuitandika KMC kwa bao 1-0, lililofungwa na David Kameta ‘Duchu’ katika dakika ya 45 ya kipindi cha kwanza bao lililodumu hadi kipyenga cha mwisho.
Kati mchezo mwingine uliochezwa leo, Ihefu iliyokuwa katika uwanja wa nyumbani ilifanikiwa kutinga hatua hiyo kwa kuifunga Pan Africa kwa mabao 2-0 yakiwafungwa na Andrew Sinchimba katika kipindi cha kwanza na pili.
Timu hizo zimeungana na nne katika hatua hizo ambazo ni Simba, Yanga, Geita Gold, Singida zilizotangua katika katika hatia hiyo baada ya kushinda michezo yao huku zikisubiri nyingine mbili ambazo zinashuka leo kusaka nafasi hizo.
Katika mchezo wa kesho Kagera Sugar ambayo itakuwa nyumbani kwenye dimba la Kaitaba itawakaribisha Mbeya City na mtanange mwingine ni dhidi ya Azam FC watakaokuwa kwenye uwanja wa nyumbani ikiwakaribisha Mapinduzi inayoshiriki Ligi ya mabingwa Daraja la Tatu.