NA MWANDISHI WETU, DAR ES SALAAM
BENKI ya Biashara ya Akiba(ACB) imeburuzwa mahakamani na mteja wake, Aisha Abubakar Hassan baada ya hati yake ya nyumba aliyoiweka dhamana ya mkopo kupotea.
Kwa mujibu wa hati ya madai aliyofungua Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam, mfanyabiashara huyo wa vipodozi alichukua mkopo wa Sh.Mil 30 katika benki hiyo Novemba 4, 2021 kwa ajili ya kupanua biashara hiyo.
Ili kupata mkopo huo uliotakiwa kurejeshwa ndani ya miezi 18 kwa riba ya asilimia 1.5 kila mwezi, Aisha aliweka dhamana ya hati ya nyumba iliyopo kitalu namba 2136, bloku H, Tegeta, wilaya ya Kinondoni Dar es Salaam.
Anadai kuwa alipomaliza mkopo huo Benki hiyo haikurejesha hati yake.
Baada ya kufuatilia mara kadhaa na kumwandikia barua mbili Meneja wa Tawi la Benki hiyo bila mafanikio, kupitia wakili wake alitoa taarifa ya kusudio la kuchukua hatua za kisheria, ndipo baadaye benki hiyo ikamjibu kuwa hati hiyo imepotea.
Kwa mujibu wa barua hiyo iliyosainiwa na meneja wa mikopo, Charles Kamoto na mwanasheria wa benki hiyo, Niwaeli Mziray, benki hiyo ilisema imeomba nakala kutoka masijala ya ardhi ya Dar es Salaam.
Hata hivyo, mfanyabiashara huyo akiwakilishwa na Wakili Peter Kibatala amefungua shauri hilo, akiiomba Mahakama iiamuru benki hiyo imrejeshee hati ya nyumba yake.
Pia anaitaka benki hiyo imlipe jumla ya Sh.Mil.355 /-kati ya hizo Sh.Mil 250/- zikiwa ni fidia ya hasara ya kukosa biashara kutokana na benki kutokumpatia hati ya nyumba hiyo na hivyo kushindwa kuiuza kwa mteja aliyekuwa tayari kumlipa kiasi hicho.
Vilevile anaiomba Mahakama hiyo iiamuru ACB imlipe fidia ya Sh100 milioni kwa hasara ya kukosa kipato alichokuwa akikitarajia kutokana na biashara yake hiyo aliyokusudia kuipanua kwa kuongeza bidhaa.
Malipo mengine ni Sh.mil 5/-ikiwa ni hasara ya malipo ya awali aliyokuwa amelipa kwa mmiliki wa chumba cha biashara (fremu), katika Mtaa wa Mchikichini na Congo, Kariakoo, Dar es Salaam.
Pia anaiomba Mahakama hiyo iiamuru benki hiyo imlipe fidia ya hasara ya jumla kwa kadiri itakavyotathmini, kwa kuendelea kushikilia hati yake wakati alishamaliza kurejesha mkopo na riba.
Vilevile anaomba riba ya asilimia 21 ya jumla ya malipo hayo yote ya fidia aliyoyataja, na riba ya asilimia ya kiwango cha mahakama kuanzia tarehe ya hukumu mpaka tarehe ya kumaliza malipo hayo na gharama za kesi.
Katika hati ya madai namba 199 ya mwaka 2023, mfanyabiashara huyo anayeagiza vipozi hivyo kutoka Uingereza, Uturuki na Marekani, na kuviuza katika duka lake lililoko Namanga, Oysterbay, anadai kwamba aliamua kuchukua mkopo kwenye taasisi nyingine ili kumaliza kulipa deni lililokuwa limesalia.
Anadai alifanya hivyo kwa matarajio kwamba akimaliza deni hilo atapewa hati yake ya nyumba ambayo alishaingia makubaliano na mteja kuinunua kwa Sh.Mil. 250/- ambazo kati yake angetumia Sh.Mil.200 /-kupanua biashara yake kwa kuagiza bidhaa hizo.
Mfanyabiashara huyo anadai kuwa bidhaa hizo alitarajia kuziuza kwa bei ya rejareja na jumla kwa wateja wa ndani na nje katika kipindi cha sikukuu za mwisho na mwanzo wa mwaka 2023.
Hata hivyo anadai benki hiyo haikuweza kumrejeshea hati yake hiyo, jambo lililofanya biashara ya kuuza nyumba hiyo kukwama na pia kushindwa kurejesha mkopo aliouchukua katika taasisi nyingine kumaliza deni hilo, hivyo deni la mkopo huo kuendelea kukua na hasa riba.
Kesi hiyo inayosikilizwa na Jaji Obadia Bwegoge imepangwa kutajwa Machi 23, kwa ajili ya kupanga utaratibu wa usikilizwaji wake.