NA MWANDISHI WETU
MBUNGE wa Jimbo la Tunduru Kusini Daimu Mpakate amesema asilimia 60 ya wananchi jimboni kwake wamenufaika na ujenzi wa minara ya simu ya Airtel inayofadhiliwa na Mfuko wa mawasiliano kwa wote (UCSAF) Tanzania nzima.
Akizungumza na Demokrasia juu ya Manufaa ya Mradi wa Minara hiyo Mbunge Mpakate alisema uwepo wa minara hiyo jimboni kwake umepokelewa vizuri kutokana na kuboreshwa kwa huduma ya mtandao wa Airtel.
Aidha Mbunge Mpakate alieleza kuwa mitandao imerahisisha kupeana taarifa mbalimbali hata za kibiashara.
Alibainisha kuwa upashanaji habari ulikuwa mgumu watu walilazimika kusafiri ili kupeana habari.
Aidha alitoa maoni juu ya mtandao wa Airtel kuboresha huduma za vifurushi iboreshwe kulingana na hali ya uchumi, viwepo vifurushi vya watu wa vijijini kulingana na hali yao ili kuongeza matumizi ya simu
Katika hatua nyingine zaidi ya sh.bilioni 6 /-zinatarajiwa kutumika katika mradi wa ujenzi wa minara ya simu yenye uwezo wa teknolojia ya 4G katika vijiji Tanzania nzima.
Ujenzi huo wa minara unaosimamiwa na Mfuko wa mawasiliano kwa wote (USCAF) awamu ya sita utasaidia kuboresha huduma mbalimbali za kidijitali zitolewazo na kampuni ya simu za mkononi ya Airtel.
Sambamba na hilo ujenzi huo utasaidia kuimarisha upatikanaji wa huduma ya mawasiliano katika katika maeneo ya vijijini hapa nchini ambapo kwa awamu iliyopita zaidi ya minara 100 ilijengwa
Miongoni mwa huduma hizo ni intaneti ya haraka , mawasiliano yasiyo ya kusuasua pamoja na huduma jumuishi za kifedha.
Baadhi ya maeneo yatakayonufaika ni pamoja na Shinyanga, Tunduru, Singida, Geita, Lindi na Mtwara.