NA MWANDISHI WETU, MBOZI
UONGOZI wa Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro (NCAA) kwa kushirikiana na Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Songwe Jumamosi Machi 4, 2023 unatarajia kufungua Makumbusho ya Kimondo yaliyopo katika Kijiji cha Ndolezi katika Wilaya ya Mbozi mkoani Songwe.
Kimondo cha Mbozi ni moja ya kivutio bora cha utalii katika Mkoa wa Songwe na ni miongoni wa vimondo vizito kumi vinavyojulikana duniani na cha pili kwa ukubwa barani Afrika.
Akitoa taarifa ya ufunguzi huo leo Machi Ofisa Uhifadhi Mkuu wa Uhusiano wa NCAA, Joyce Mgaya amesema ufunguzi wa Makumbusho hayo ni miongoni mwa hatua za kuunga mkono jitihada za Serikali katika kukuza Utalii katika mikoa ya Nyanda ya juu Kusini na pia kuimarisha uhifadhi wa urithi tulionao wa mila na tamaduni zetu.
”Ufunguzi wa Makumbusho hii ni fursa ya kujivunia na kuenzi tamaduni hususan wananchi wa Mkoa wa Songwe. Nawaomba wakazi wa Mkoa wa Songwe mjitokeze kwa wingi kushuhudia ufunguzi huo “amesema Mgaya
Amefafanua kuwa kukamilika kwa Makumbusho licha ya kuhifadhi taarifa za kimondo hicho pia Makumbusho hiyo itasaidia kuhifadhi mila na tamaduni za makabila ya watu wa Nyanda za Juu Kusini hususan kabila Wanyiha, Ndali na Wanyamwanga.
Ofisa huyo wa Uhusiano ameongeza kuwa siku ya kesho wageni mbalimbali wa ngazi ya Taifa, mkoa, na wilaya wanatarajia kushiriki katika ufunguzi huo ikiwemo Bodi ya Wakurugenzi wa NCAA wakiongozwa na Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi Jenerali Venance Mabeyo ( Mstaafu).
Aidha, Mgaya amesema mara baada ya ufunguzi wa Makumbusho hayo kutafuatia na tukio la kutembelea program maalum ya elimu ya anga pamoja na kutembelea kivutio kingine cha utalii cha maji moto kilichopo katika eneo la Nanyala.
Kimondo cha Mbozi kiligunduliwa na Mwafrika aliyejulikana kwa jina la Mzee Halele ambaye alikuwa Mhunzi hivyo katika harakati zake za kutafuta chuma alikiona kimondo hicho na baadae kumbukumbu za kimondo hicho ziliwekwa kwenye maandishi na Mzungu aliyeitwa Wiliam Nolt mwaka 1930.