NA EDNA BONDO
MACHI 8 ya kila mwaka wanawake duniani kote huadhimisha siku yao. Mojawapo ya mambo makuu katika maadhimisho ya siku hii adhimu ni kuangazia mafanikio ambayo wanawake wamekuwa wakiyapata aidha kwa kuwezeshwa ama kujiwezesha.
Kauli mbiu ya mwaka huu ni Ubunifu na Mabadiliko katika teknolojia chachu ya kuleta usawa wa kijinsia mbayo inakwenda sambamba na miradi ya kujiendeleza kielimu kwa njia ya mtandao iitwayo VSOMO.
Aidha kauli mbiu ya mwaka huu inawiana na mada ya kipaumbele cha Kikao kijacho cha 67 cha Tume ya Hali ya Wanawake (CSW-67).
VSOMO ni Ushirikiano wa Airtel Tanzania katika kutoa fursa ya kupata kozi za Ufundi Stadi zinazotolewa na Mamlaka ya Mafunzo ya Ufundi Stadi (VETA) kupitia Program ya simu yenye lengo la kusaidia nchi kupata mafunzo ya ufundi stadi kupitia jukwaa la simu.
Tangu 2016, jukwaa la VSOMO limekuwa likitoa kozi nyingi za ufundi ambazo ni pamoja na upishi, ufundi pikipiki, uwekaji umeme, fundi simu za rununu, urembo, uchomeleaji na utengenezaji wa chuma, aluminiamu muundo wa usanifu wa Upvc, na matengenezo ya kompyuta kati ya zingine.
VSOMO inaendana na ajenda ya Serikali ya kutengeneza fursa za ajira kwa vijana. Zaidi ya wasichana 504 wameidhinishwa katika kozi 16 tofauti zinazotolewa kupitia aplikesheni ya VSOMO inayofadhiliwa na Airtel.
Mbali ya hayo , Ubunifu na mabadiliko ya teknolojia, na elimu katika zama za kidijitali kwa ajili ya kufikia usawa wa kijinsia na uwezeshaji wa wanawake wote na wasichana hivyo mpango wa Airtel VSOMO unalenga kukuza uwekaji kidijitali nchini na kwa sababu ya urahisi, kunyumbulika, na uwezo wa kumudu.
Mpango huu umekuwa ukiwavutia maelfu ya vijana mwaka hadi mwaka zaidi ya vijana 51,000 wamepakua programu, 21,000 wamesajiliwa. , 1,260 wameandikishwa na kuthibitishwa.
Takriban asilimia 80 ya wanafunzi waliohitimu wana umri wa kati ya miaka 18 hadi 35 ambao takwimu zinaonesha kuwa wengi ni wanawake.
“Tulipoanzisha VSOMO na Mamlaka ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi, wazo lilikuwa kutoa mafunzo kwa vijana zaidi katika fani mbalimbali mtandaoni nchini kote,” anasema Mkurugenzi wa Mawasiliano wa Airtel Tanzania, Beatrice Singano.
Julai mwaka huu, VSOMO, programu ya simu inayotoa kozi fupi za mafunzo ya ufundi kupitia simu ya mkononi, itakuwa ikitimiza miaka saba tangu kuanzishwa kwake ikilenga kuongeza wigo wa upatikanaji maarifa nchini.
Pamoja na kwamba Vsomo ni moja ya programu chache za kibunifu nchini zinazolenga kuongeza ujuzi miongoni vya vijana hasa wakati nchi ikijikita kuwekeza katika uchumi wa viwanda, ni wachache wanafahamu umuhimu wake
Happiness Shayo ni miongoni mwa wanawake walionufaika na VSOMO ambaye hivi sasa amejiajiri katika biashara ya ushonaji baada ya kuhitimu. Anasema mwanzoni hakuwa na ujuzi wowote, alijipatia ujuzi wa ushonaji kupitia Airtel VSOMO ambapo sasa hivi amefungua biashara yake ndogo ya ushonaji .
“Ninaweza kujitunza vizuri mimi na familia yangu kwa mapato ninayopata kutokana na biashara hii. Kama mwanamke, nina furaha kwamba ninaweza kuendesha maisha yangu kwa biashara ambayo nimeanzisha. Asante sana Airtel na VETA kwa fursa hii”.
Mnufaika wa pili VSOMO , Doreen Kimolo anaieleza Demokrasia kuwa “Nilikuwa tu mwanamke ambaye nakaa nyumbani. Nilipenda kujiunga na kozi ya kuoka keki kwa sababu niliamini kuwa naweza kuendesha biashara zangu nyumbani. Unajua wanawake wengi wanajihusisha na kazi za nyumbani ambazo zinatuzuia kufanya shughuli fulani za kiuchumi. Shukrani kwa Airtel na VETA kwa kuanzisha programu hii ya VSOMO kwa sababu nilifanikiwa kusoma nikiwa nyumbani bila kuathiri majukumu yangu mengine kama mwanamke.”
” Nilijiunga na Kituo cha VETA kwa muda mfupi sana kwa ajili ya kikao cha vitendo. Sasa ninaendesha biashara yangu ya keki nyumbani. Napokea oda kutoka mitandao ya kijamii ya facebook na instagram, naandaa oda na kutumia bodaboda iliyopo kuwapelekea keki wateja wangu. Nawahimiza wanawake wengine kujiunga na VSOMO ili kupata ujuzi, kujiamini zaidi katika maisha na kuanzisha biashara zao ndogo ndogo”
VSOMO INAFANYAJE KAZI?
Sospeter Mkasanga ni Mkuu wa Chuo TEHAMA VETA Kipawa, kituo kunachosimamia utekelezaji wa Mradi wa VSOMO nchini. Anasema Vsomo inatoa mafunzo ya kozi fupi za ufundi za Veta za wiki nane ndani ya kipindi kifupi tu kisichozidi wiki nne kwa kutumia simu ya mkononi.
Msomaji anatakiwa kupakua aplikesheni hiyo kutoka kwenye Play store kwa wanaotumia simu za Android na kisha kujisajili kwa kutumia laini ya simu ya Airtel.
Sifa kubwa anayejiunga na kozi hiyo ni awe na uwezo wa kusoma na kuandika na awe na uhakika wa kuipata simu janja (smartphone) wakati wote ili kumsaidia kujifunza nadharia ambayo sehemu kubwa ni maandishi na picha.
Kwa anayejisajili anaweza kuona tu kozi zilizopo na maudhui yake bila kuweza kusoma kozi yenyewe mpaka atakapolipia ada ya Sh.120,000 kupitia Airtel Money ambayo inajumuisha hadi gharama za mafunzo kwa vitendo.
Wastani wa ada ya kozi fupi zinazotolewa na Veta kwa mujibu Mkasanga ni kati ya Sh.250,000 hadi Sh320,000 kwa kozi hivyo kufanya Vsomo kuwa nafuu zaidi ya mara mbili ya gharama ya kawaida.
Wanafunzi wa ufundi wakifanya majaribio ya kazi zao. VSOMO inatoa fursa ya wiki mbili kujifunza kwa vitendo kwa yule aliyemaliza masomo ya nadharia kupitia simu ya mkononi. Picha kwa hisani ya Vsomo.
Mwanafunzi anayesoma kupitia VSOMO atasoma nadharia ya kozi husika na kufanya mitihani yote na kufanya miadi katika chuo cha Veta kilichopo jirani kwa ajili ya kufanya mafunzo ya vitendo kwa saa 60 ndani ya wiki mbili.
“Mtu anayesoma kupitia Vsomo anakuwa na uhuru na muda wake na anapunguza gharama za masomo. Ukiamua kusoma kwa siku mbili au mwezi au miezi mitatu sawa tu ilimradi mitihani yote ufaulu,” anasema Mapuli.
Uhuru huo, kwa mujibu wa Mkasanga ndiyo unaowafanya hata watu waliopo shuleni au kazini wasome mafunzo ya ufundi kuongeza ujuzi wa kujiongezea kipato.
Kuna kozi 16 katika aplikesheni hiyo ambazo hutolewa na Veta nchini zikiwemo ufundi umeme wa majumbani, umeme wa viwanda, ufundi wa simu za mkononi, urembo na upishi.
MCHAKATO WA KUDHIBITI UBORA
Ili kukabiliana na udanganyifu katika mafunzo hayo, Mkasanga anasema kuwa kabla ya mwanafunzi kufanya mafunzo ya vitendo karibu na chuo cha Veta cha karibu hutakiwa kufanya mtihani wa ana kwa ana ambao utajumuisha pia maswali ambayo aliyowahi kuyafanya kupitia simu ya mkononi.
“Akifaulu mtihani huo na kwa kutumia taarifa muhimu tulizonazo wakati wa usajili tutajua ni yule aliyejisajili kwenye app,” anasema.
Mwanafunzi anayemaliza katika mafunzo hayo hupewa cheti sawa kabisa na yule aliyesoma kozi fupi ya wiki nane katika chuo chochote cha Veta nchini.
Mkasanga anasema wahitimu wa kozi hizo wanatambulika na kuajiriwa na mamlaka mbalimbali nchini zikiwemo Mamlaka ya udhibiti wa huduma za nishati na maji (Ewura), Shirika la ugavi wa umeme Tanzania (Tanesco) na Wakala wa nishati vijijini (Rea) na nyinginezo.