NA MAGENDELA HAMISI, DAR ES SALAAM
MSHAMBULIAJI wa zamani wa Klabu ya Simba, Madaraka Seleman ‘Mzee wa Kiminyio’ ametoa wito kwa wachezaji wa timu hiyo kubeba msalaba kwa kuhakikisha wanashinda mchezo wa februari 25, 2023 wa Klabu Bingwa Afrika dhidi ya Vipers FC ya Uganda.
Mwanandinga huyo mkongwe, akizungumza na Demokrasia alisema kuwa mchezo huo ni mgumu hivyo wachezaji wanatakiwa kuhakikisha wanapata ushindi kwa maana wakipoteza matumaini ya kusonga mbele katika michuano hiyo itakuwa imepotea.
Wachezaji wanatakiwa kufanya wafanyavyo kuhakikisha wanatapa ushindi kwa kutumia kila nafasi wanayoipata uwanjani kufunga , naamini kocha amemaliza kazi yake kilichobaki ni kwa wachezaji kuuchukulia mchezo huo kama fainali kwa maana wao ndio wapo mstari wa mbele,” alisema.
Nyota huyo mkongwe aliyekuwa na kikosi cha Simba kilichoshiriki michuano ya Kombe la CAF na kutinga fainali mwaka 1993, pia aliwashauri wanachama na mashabiki wa klabu hiyo kwa sasa kutulia na si kuanza kurusha maneno yasiyofaa kwa viongozi baada ya timu kutopata matokeo mazuri katika michuano hiyo.
Wanachama na mashabiki kulalamika pindi timu inapofanya vibaya ni kawaida katika mpira na ninachowaomba wawape muda viongozi kwa maana timu bado haijashindwa na kama ikishindwa ndio wapeleke malalamiko ili mabaya yafanyiwe kazi,” alisema
Klabu ya Simba baada ya kuanza michezo ya hatua ya makundi imeshacheza michezo miwili, wa ugenini dhidi ya Horoya AC ambayo ilipoteza kwa bao 1-0 na wa pili ilicheza nyumbani ambapo ilipoteza kwa idadi kubwa ya mabao 3-0 dhidi ya Raja Casablanca ya Morocco.
Hadi sasa Simba inashika nafasi ya mwisho katika kundi lao huku Vipers ikishika nafasi ya tatu ikiwa na alama moja, Horoya inashika nafasi ya pili ikiwa imejikusanyia alama nne kibindoni na wanaongozwa na Raja wenye alama sita na timu zote zikiwa tayari zimeshuka dimbani mara mbili na michezo minne imesalia kwa kila timu