NA MWANDISHI WETU, NJOMBE
KUNDI la watu wanaodhaniwa kuwa ni majambazi wakiwa na silaha za moto na jadi wamevamia na kuteka magari zaidi ya 7 majira ya Saa mbili usiku katika mlima Nyalivi katikati ya Kijiji cha Kidegembye na Nyombo wilayani Njombe na kisha kupora fedha, simu na Mali nyingine za abiria.
Wakisimulia tukio hilo wakiwa hospitalini baadhi ya majeruhi Mwamini Hongoli na Benard Kawogo ambaye ni dereva wa basi la abiria wamesema watekaji waliangusha mti na kisha kulazimisha watu kutoa fedha huku sura zao zikiwa zimefunikwa na maski.
Kawogo amesema punde baada ya gari lao kushikiliwa na kisha kuanza kushinikizwa kutoa fedha ,alijaribu kukimbia jambo ambalo lilisababisha kupigwa mapanga kichwani na mgongoni.
Kufuatia majeruhi waliokeruhiwa kwa mapanga na kupelekwa katika vituo tofauti vya afya huku wenye majeraha makubwa wakipelekwa hospitali ya Halmashauri ya mji wa Njombe Kibena ,Demokrasia ilifika Hospitali ya Kibena na kufanya mahojiano na kaimu mganga mfawidhi Dk Ayoub Mturo ambaye amekiri kupokea wagonjwa na kuwapa matibabu
Kamanda wa Jeshi la Polisi mkoa wa Njombe Hamis Issa amethibitisha kutokea kwa tukio hilo na kwamba jeshi la polisi linaendea kufuatilia wahusika wa tukio hilo ili wakamatwe ili sheria ichukue mkondo wake.
Katika hatua nyingine, Nasson Simbila ni mmiliki wa basi lililotekwa na kisha kuvunjwa kioo na majambazi hao, wakati wa kurupushani,amesema ni tukio ambalo limesababisha hasara kubwa kwenye gari lake hali ambayo itagharimu matengenezo Kwa gharama kubwa hivyo kuliomba jeshi la polisi kushirikiana na wananchi Ili kuwakamata waharifu hao