NA TERESIA MHAGAMA,DAR ES SALAAM
NAIBU Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dk Doto Biteko
amempongeza na kumshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,
Dk. Samia Suluhu Hassan kwa juhudi zake za kustawisha ustawi wa
kidemokrasia nchini, sambamba na kuimarisha miundombinu ya kiuchumi na
kijamii ili kuwaletea Maendeleo watanzania.
Dk Biteko amesema hayo leo Januari 4, 2024 jijini Dar es Salaam
wakati akifunga Mkutano Maalum wa Baraza la Vyama vya Siasa nchini
ulioshirikisha wadau wa Demokrasia ya Vyama vingi vya Siasa ili
kujadili miswada ya Sheria za Uchaguzi na Muswada wa Sheria za Vyama
vya Siasa.Mkutano umeandalilwa na Baraza la Vyama vya Siasa.
Miswada iliyokuwa ikijadiliwa ni muswada wa Sheria ya Uchaguzi wa
Rais, Wabunge na Madiwani wa mwaka 2023, Muswada wa Sheria ya Tume ya
Uchaguzi wa mwaka 2023 na Muswada wa Sheria ya Marekebisho ya Sheria
za Vyama vya Siasa wa mwaka 2023.
“ Rais wetu amekuwa ni mfano wa kuigwa, kitaifa na kimataifa kwa
kuhakikisha kuwa Demokrasia yetu inazidi kustawi na kuifanya Serikali
kuendeshwa kwa misingi ya haki, utawala bora na kwa mujibu wa sheria
tulizojiwekea na bila kusahau kuzingatia maoni ya watu ambao ni muhimu
katika kuboresha utendaji wetu.” amesema Dk. Biteko
Dk. Biteko amepongeza Baraza la Vyama vya Siasa kwa kuandaa mkutano
huo ambao ni muhimu kwa maslahi ya Taifa na kueleza kuwa Baraza hilo
kwa kwa mujibu sheria linajukumu pia la kuishauri Serikali kuhusu
utekelezaji wa sheria ya vyama vya siasa na masuala mengine yanayohusu
vyama vya siasa na Demokrasia.
Amesema kuwa, mkutano huo umekuwa wenye tija kwani washiriki wameweza
kutoa maoni yao kwa kuzingatia maslahi ya nchi.
Katika hatua nyingine, Dk. Biteko amewaasa wajumbe wa Mkutano huo
kuitikia wito wa Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,
Dk. Tulia Ackson wa kwenda bungeni kuanzia Januari 6 hadi 10 mwaka huu
ili kutoa maoni kuhusu miswada ya sheria za uchaguzi na mswada wa
sheria ya vyama vya siasa.
Amewashukuru wajumbe hao kwa kutoa maoni ambayo ni bora na kwa
kujadiliana kwa uungwana kuhusu miswada hiyo, kwani hakuna chama
kilichoonesha kuwa kina umiliki wa kutoa mawazo bali wote
walisikilizana huku akieleza kuwa yale waliyojadiliana itakuwa ni
muendelezo wa kujenga maridhiano ya kitaifa.
Kuhusu sheria zilizopo nchini amesema kuwa, endapo kuna sheria
inaonekana ina changamoto baada ya kuitumia kwa muda mrefu, “wito wa
Dk.Samia Suluhu Hassan ni sote kukaa na kuridhiana kama Taifa wapi
tuboreshe na Bunge ni Taasisi mahiri yenye uongozi mahiri ambao
watapokea maoni yetu na kuyafanyia kazi na mahali ambapo Serikali
itapaswa kupeleka muswada sheria ya marekebisho bungeni itafanya
hivyo.”
Awali, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge na Uratibu,
Jenista Mhagama, amesema kuwa, lengo la mkutano huo lilikuwa ni
kukutanisha wadau wengi wanaohusika na masuala ya demokrasia ya mfumo
wa vyama vingi nchini ili kutoa maoni yatayoboresha miswada kwa
kupitia utaratibu utakaozingatia sheria na kanuni za upitishwaji wa
miswada katika Bunge la Tanzania.
Amesema kuwa, mkutano huo umekuwa na mafanikio makubwa na wadau
wametoa maoni yao kwa amani na ushirikiano mkubwa, hivyo amepongeza
Baraza la Vyama vya Siasa, kwa kuandaa mkutano huo na kusema kuwa,
Serikali itaendelea kuliunga mkono Baraza hilo katika utekelezaji wa
mipango yake.
Kwa upande wake, Msajili wa Vyama vya Siasa, Jaji Francis Mutungi
amesema kuwa, zao la mkutano huo ni muongozo uliotolewa na Rais, Dk
Samia Suluhu Hassan wakati alipopokea taarifa ya kikosi kazi
alichokiunda cha kuratibu maoni ya wadau wa Demokrasia ya vyama vingi
vya siasa ambapo moja ya masuala aliyoelekeza ni kufanyika kwa
maboresho ya sheria za uchaguzi na sheria za vyama vya siasa.
Amemshukuru Rais kwa jitihada zake katika kukuza na kuendeleza
demokrasia nchini kwani kukutana kwa Baraza hilo kunatokana jitihada
hizo za uwepo wa demokrasia nchini.
Viongozi mbalimbali waliohudhuria Mkutano huo ni pamoja na Waziri wa
Nchi, Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais Zanzibar, Hamza Hassan Duma,
Mkuu wa Mkoa wa Da es Salaam, Albert Chalamila na Naibu Spika wa
Baraza la Wawakilishi Zanzibar, Mgeni Hassan Juma.