NA JANETH JOVIN,DAR ES SALAAM
RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk.Hussein Ali Mwinyi, amewahimiza wafanyabiashara wa Tanzania kutumia kikamilifu fursa zinazotolewa na Soko Huru la Biashara la Afrika (AfCFTA) pamoja na utaratibu wa biashara usio na ushuru (zero tariff) katika baadhi ya nchi jirani ili kupanua masoko ya bidhaa zinazozalishwa nchini na kuongeza ushindani wa uchumi.
Akifunga Maonesho ya 50 ya Biashara ya Kimataifa ya Dar es Salaam (Sabasaba), Dk. Mwinyi alisema Serikali itaendelea kuweka mazingira wezeshi yatakayochochea ukuaji wa sekta za biashara na viwanda, huku akizitaka taasisi za umma kuondoa urasimu unaochelewesha utoaji wa huduma kwa wananchi na wawekezaji.
“Tumeendelea kuweka mkazo mkubwa wa kuhamasisha Watanzania kutumia fursa mbalimbali zilizopo, ikiwemo Soko Huru la Biashara la Afrika na utaratibu wa zero tariff katika nchi jirani ili kupanua masoko ya bidhaa zinazozalishwa hapa nchini,” alisema.
Alisema mafanikio ya maendeleo ya taifa yanategemea utekelezaji wa vipaumbele vya kitaifa kwa vitendo, nidhamu na uwajibikaji, huku akisisitiza kuwa Serikali itaendelea kusimamia mazingira bora ya biashara na uwekezaji ili kuleta matokeo chanya kwa uchumi wa nchi.
Dk. Mwinyi alisema Maonesho ya Sabasaba yameendelea kuwa jukwaa muhimu linalowakutanisha wawekezaji, wazalishaji na wafanyabiashara kutoka ndani na nje ya nchi, sambamba na kutoa nafasi kwa Watanzania kuonesha ubunifu, teknolojia na bidhaa zenye ubora zinazoweza kushindana katika masoko ya kimataifa.
Alibainisha kuwa programu mbalimbali zilizoendeshwa wakati wa maonesho hayo zimeongeza uelewa kuhusu fursa za biashara, uwekezaji na maendeleo ya uchumi, hatua inayochangia kujenga uchumi wa kisasa na wenye ushindani.
Aidha, aliitaka Mamlaka ya Maendeleo ya Biashara Tanzania (TanTrade) kuendelea kutafuta masoko mapya na kuboresha huduma wezeshi ili kuwasaidia wafanyabiashara wa Tanzania kunufaika zaidi na fursa za biashara ndani na nje ya nchi.
Kwa upande wa taasisi za Serikali, Dkt. Mwinyi alisema zina wajibu wa kuhakikisha zinaondoa vikwazo vya kiutendaji, kuimarisha uwazi na uwajibikaji pamoja na kusimamia matumizi sahihi ya rasilimali za umma ili kuboresha utoaji wa huduma.
Akihitimisha hotuba yake, aliwapongeza washiriki wa Maonesho ya 50 ya Biashara ya Kimataifa ya Dar es Salaam kwa ushiriki mkubwa wa taasisi za ndani na nje ya nchi, akisema hatua hiyo imepanua fursa za biashara na kuimarisha ushirikiano wa kiuchumi.
Pia aliipongeza TanTrade kwa uratibu wa maonesho hayo na kuitaka kuendeleza mafanikio yaliyopatikana kwa kuboresha maeneo yenye changamoto ili kuongeza ufanisi wa maonesho hayo katika miaka ijayo.
Naye Waziri wa Viwanda na Biashara, Judith Kapinga, amesema maonesho ya sabasaba yameidhihirisha nafasi ya Tanzania kama kitovu cha biashara, uwekezaji na uzalishaji barani Afrika, huku akisisitiza kuwa maonesho hayo yanapaswa kuwa lango la kudumu la biashara badala ya kuwa tukio la kila mwaka pekee.
Akizungumza katika hafla hiyo ya kufunga maonesho hayo, Kapinga alisema miaka 50 ya Sabasaba ni ushahidi wa safari ya Tanzania katika kujenga uchumi unaotegemea uzalishaji, biashara bunifu na ushirikiano wa kimataifa.
Alisema kwa zaidi ya nusu karne, Sabasaba imeendelea kuwa daraja linalowaunganisha wazalishaji, wafanyabiashara, wawekezaji, wabunifu, taasisi za fedha na masoko ya ndani na nje ya nchi, jambo lililoifanya Tanzania kuwa kitovu muhimu cha biashara Afrika Mashariki na Kusini.
“Mwaka huu tumeshuhudia Sabasaba yenye mafanikio makubwa zaidi. Maonesho haya yamefungua milango ya mikataba mipya ya biashara, yameimarisha ushirikiano kati ya sekta binafsi na serikali na yameendelea kuthibitisha kuwa Tanzania ni kitovu cha fursa za biashara na uwekezaji barani Afrika,” alisema.
Kapinga alisema kwa wafanyabiashara, Sabasaba imekuwa zaidi ya maonesho kwani imegeuka kuwa darasa la biashara, soko la bidhaa, jukwaa la ubunifu na sehemu ya kujenga mahusiano ya muda mrefu ya kibiashara.
Alibainisha kuwa kwa wawekezaji, maonesho hayo yamekuwa dirisha la kuona fursa zilizopo katika sekta za viwanda, kilimo, madini, utalii, huduma na uchumi wa kidijitali, huku kwa vijana yakithibitisha kuwa ubunifu unaweza kubadilishwa kuwa biashara zenye ushindani wa kimataifa.
Aidha Kapinga alisisitiza umuhimu wa kuifanya kaulimbiu ya “Made in Tanzania” kuwa ajenda ya kitaifa ya maendeleo ya uchumi badala ya kubaki kauli inayotumika wakati wa maonesho pekee.
“Made in Tanzania ni alama ya ubora, uaminifu, usalama na ushindani wa bidhaa zetu. Huo ndiyo msingi wa kuzifanya bidhaa za Tanzania zipenye na kushindana katika masoko ya dunia,” alisema.






