NA MWANDISHI WETU, DAR ES SALAAM
KUTOKANA na ongezeko la mahitaji ya huduma za matibabu ya moyo nchini, Rais wa Tanzania Samia Suluhu Hassan ametoa kiasi cha Sh. Bilioni 3.6 kwa lengo la kujenga jengo la utawala na vipimo ikiwa ni sehemu ya kuboresha huduma zinazotolewa na Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI).
Jengo hilo linalotarajiwa kumalizika Agosti mwaka huu linatarajiwa kutoa huduma za vipimo kwa wagonjwa wa moyo na magonjwa yasiyoambukiza zaidi ya 200 kwa siku hivyo kupunguza muda wa kusubiri huduma za vipimo na matibabu.
Hayo yamebainishwa hivi karibuni na Katibu Mkuu Wizara ya Afya Dk. Seif Shekalaghe wakati alipotembelea JKCI kwa lengo la kuangalia maendeleo ya ujenzi wa jengo hilo ambalo limefikia asilimia 71 kukamilika.
Akizungumza na waandishi wa habari mara baada ya kukagua jengo hilo, Dk. Shekalaghe alisema jengo moja la JKCI lililopo kwa sasa linahudumia wagonjwa wa nje, linatoa huduma za vipimo, kutoa huduma za upasuaji wa moyo pamoja na kulaza wagonjwa hivyo kuleta msongamano mkubwa kwa wagonjwa wanaopata huduma hospitalini hapo.
Alisema ili kuondoa changamoto hiyo Rais Samia ameamua kutoa kiasi hicho cha fedha kwa lengo la kufanya maboresho hayo ambayo yatasaidia wagonjwa wengi kupata huduma kwa wakati.
“Wizara inafuatilia hela zinazotolewa na Rais ziweze kukidhi mahitaji yaliyokusudiwa kwa wakati hivyo tunawataka wakandarasi wa ujenzi huo kufanya kazi usiku na mchana ili ujenzi uweze kukamilika, Rais anapenda anapotoa fedha zitumike kama zilivyopangwa ili aweze kutoa tena zingine katika kuboresha sekta ya afya,” alisema Dk. Shekalaghe.
Aidha Dk. Shekalaghe alimtaka Mkurugenzi Mtendaji wa JKCI, Dk. Peter Kisenge kuhakikisha kuwa vifaa vinavyohitajika katika jengo hilo vinaandaliwa mapema ili linapokamilika mwezi wa nane lianze kutumika hapo hapo na kusiwe na changamoto za kusubiria vitendea kazi
Kwa upande wake Mkurugenzi wa JKCI, Dk. Kisenge alisema wagonjwa wa moyo wamekuwa wakisubiri kwa muda mrefu kupata huduma za vipimo vya moyo hivyo kumalizika kwa jengo hilo kutawapa nafuu wagonjwa kutokusubiri huduma za vipimo hasa cha kuangalia jinsi moyo unavyofanya kazi (Echocardiograph – ECHO).
“Mitambo itakayowekwa katika jengo hili l itakuwa mikubwa na ambayo inachukua muda mfupi kutoa huduma za vipimo na majibu, tunatarajia ndani ya masaa mawili mgonjwa anaweza kuwa ameshafanyiwa vipimo, kupatiwa majibu yake na kumuona daktari”, alisema Dk. Kisenge
Aidha Dk. Kisenge alisema jengo hilo la utawala na vipimo litatoa huduma za maabara, huduma za vipimo vya ECHO na ECG, eneo maalum kwa ajili ya wagonjwa wanaotoka nje ya nchi pamoja na vyumba vya madaktari kwa ajili ya kuwaona wagojwa ili kuwapunguzia mzunguko.
Naye Mkandarasi wa jengo hilo kutoka Shirika la Nyumba la Taifa (NHC), Baraka Killungu alisema jengo hilo lenye ukubwa wa mita za mraba 1400 lina ghorofa nne ambapo kila ghorofa lina ukubwa wa mita za mraba kati ya 290 hadi 330.