NA MWANDISHI WETU, DAR ES SALAAM
WAZIRI wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dk.Angeline Mabula amewatuliza wapangaji wa Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) eneo la kariakoo na kuwataka kufuata sheria na mikataba walioingia na shirika hilo.
Dkt Mabula amekuatana na wapangaji hao jijini Dar es Salaam leo Juni 19, 2023 kusikiliza kilio cha wapangaji hao waliotaka kuongezewa muda wa notisi ya miezi mitatu waliopewa na NHC kupisha uwekezaji.
Aidha, wapangaji hao wameitaka serikali kupitia Shirika la Nyumba la Taifa kuwapa kipaumbele cha kuwapangisha kwenye majengo wanayoishi na kuyatumia sasa mara mradi wa uboreshaji utakaofanywa na mbia kukamilika.
Kwa mujibu wa wapangaji hao wa eneo la Kariakoo, hawapingani na uwekezaji unaofanywa na serikali bali wanachotaka ni kushirikishwa, kuongezewa muda wa notisi sambamba kupewa kipaumbele cha kupangishwa pale mradi utakapokamilika.
Akijibu maombi ya wapangaji hao, Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dk. Mabula amewaambia wapangaji hao kuwa, katika suala la uendelezaji milki, Kariakoo ni eneo litakalofanyiwa maboresho makubwa na halitarudi katika hali yake ya sasa bali itakuwa na maboresho ya majengo.
Hata hivyo, amewaambia kuwa, hakuna mkataba uliosainiwa na mbia wala muundo wa majengo uliowekwa na Shirika la Nyumba la Taifa ambapo ameweka wazi kuwa wanaodai kupewa ubia na kuanza kukusanya fedha ni matapeli wanaotakiwa kuchukuliwa hatua.
‘’Kwanza nashangaa mtu kujiita mbia na kuanza kukusanya fedha hata kabla ya kuwa na uhakika unayekusanya pesa zake atakuwa mpangaji’’. amesema Dk Mabula
Kwa mujibu wa Dk. Mabula, mkataba ulioingiwa baina ya Shirika la Nyumba la Taifa na Wapangaji una kila kitu na mpangaji anatakiwa kukijua ambapo aliwataka wanasheria wanaowashauri wateja wao kuhakikisha wanawashauri kwa kuzingatia mikataba badala ya kuwapa matumaini na kuleta taharuki.
Kwa upande wao, wafanyabiashara wamesema hawapingani na serikali katika suala zima la ubia bali wanachotaka ni kupatiwa nafasi kutokana na maeneo kuwa machache na kuweka wazi kuwa kuhamishwa kwao haraka itawawia vigumu kupata nafasi maeneo mingine huku baadhi yao wakiwa na mikopo benki hivyo wameomba kuongezewa muda wa notisi.
‘’Sisi tuko na serikali na dhamira hawapingani na serikali na tumewakataza wale wote waliokuwa na dhamira tofauti na serikali katika kutafuta mbia wa kuwekeza kwenye eneo la kariakoo’’ wamesema
Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) Hamad Abdallah amesema, anachofurahishwa ni kwamba serikali na wapangaji wa eneo la kariakoo wanakubaliana na uendelezaji unaotaka kufanyika na tofauti ni namna ya eneo hilo linavyoendelezwa.
‘’Kwa kweli hapa nashukuru sana serikali na wapangaji wa eneo la kariakoo tuna dhana moja ya kukubali kariakoo kuendelezwa’’. amesema Abdallah
Kufuatia maombi ya wapangaji hao, Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dk.Mabula ameongeza muda wa notisi kutoka miezi mitatu hadi miezi sita ambapo sasa wapangaji hao watalazimika kupisha uboreshaji kufikia Desemba 31, mwaka huu na kusisitiza fursa iliyotolewa ni kwa wafanyabiashara wa kariakoo pekee na haitatumika kwa maeneo mengine ambayo ubia wa aina hiyo utafanyika.
Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) hivi karibuni lilingia katika sera ya ubia na watu binafsi sera yenye lengo la kuendeleza ama kuboresha majengo ya shirika hilo na kuyafanya kuwa ya kisasa na yenye muonekano wa kuvutia na hatimaye kuliongezea kipato shirika hilo.