NA MWANDISHI WETU, MOROGORO
VIONGOZI wa vyama vya wafanyakazi nchini, wametakiwa kuwafikia wanachama wao kwa wakati pindi wanapopata shida ili kuepusha migogoro isiyokuwa na lazima.
Rais wa Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi (TUCTA), Tumaini Nyamuhokya amesema hayo wakati wa mafunzo kwa watendaji wa vyama vya wafanyakazi, waajiri na mashirikisho yaliyofanyika mkoani Morogoro.
Amesema ili vyama viweze kufanikisha hilo inabidi viwe na nguvu kubwa kiuchumi, ili wanachama wafikiwe kwa wakati na muda wowote wanaohitaji msaada.
” Tuwe na nguvu ya vyama vya wafanyakazi kutawanyika nchi nzima na ili hili lifanikiwe lazima tuwe imara,” amesema.
Katika hatua nyingine alisema vyama vingi vya wafanyakazi vinaanguka kutokana na migogoro inayoibuka.
” Migogoro ya ndani kwa ndani tujitahidi kuitatua ili kujenga chama,” amesema.
Naye Mwakilishi kutoka Chama cha Waajiri Tanzania (ATE), Leonard Selestine amesema suala la afya mahala pa kazi ni muhimu kwani linaongeza tija na uzalishaji.
” Niwakumbushe wafanyakazi kutimiza wajibu wenu mahali pa kazi kwa uadilifu mkubwa,” amesema.
Pia aliwataka wafanyakazi kuepuka vitendo na vishawishi vinavyosababisha rushwa mahali pa kazi, kujali muda kwa wakati sahihi na kutekelezamajukumu ya kazi.
“Waajiri wana matarajio makubwa kutoka kwa wafanyakazi, na wafanyakazi wana matarajio makubwa kutoka kwa waajiri,” amesema.
Awali Msajili wa Vyama vya Wafanyakazi nchini, Pendo Berege alisema mpaka sasa idadi ya vyama vya wafanyakazi nchini ni 33, kati ya hivyo 30 vimetuma wawakilishi isipokuwa vitatu.
Amesema wameita vyama hivyo kwa ajili kukumbusha wajibu wa wafanyakazi na kufanya tathmini.
” Ninaamini ukimwelimisha kiongozi wa chama cha wafanyakazi anawakilisha mpaka kwenye tawi lake,” amesema.
Amesema kwa mafunzo hayo yanapunguza migogoro ambayo haipaswi kuwepo kwenye maeneo ya kazi, eneo la kazi libaki ni eneo la kuzalisha.