NA MWANDISHI WETU, DAR ES SALAAM
RAIS Mstaafu wa Awamu ya Nne wa Tanzania ambaye pia ni Mkuu wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam,(UDSM) Jakaya Kikwete anatarajia kuwa mgeni rasmi katika uzinduzi wa maadhimisho ya miaka 50 ya UDSM Ndaki ya Uhandisi na teknolojia.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam, Mkuu wa Idara ya Uhandisi Umeme, Dk Francis Mwasilu amesema maadhimisho hayo yatahudhuliwa na wahandisi na wadau mbalimbali kutoka ndani na nje ya nchi.
“Malengo ya maadhimisho hayo ni kuimarisha uhusiano kati ya CoET na wadau wengine hususani viwanda, hii ni kwa sababu tunathamini sana mchango wa viwanda, waajiri wahitimu wetu katika kuboresha taaluma na huduma zetu,” amesema Mwasilu.
Amesema anaamini ushirikiano katika kuongeza matumizi ya sayansi, na teknolojia na ubunifu unaweza kuchochea zaidi ushindani katika uzalishaji na usambazaji wa bidhaa na huduma.
“Majadiliano katika maadhimisho haya yatatumika kuboresha mitaala ya kufundishia wakati UDSM itakapofanya mapitio ya mitaala hivi karibu, majadiliano hayo yatachangia katika kuainisha vipaumbele katika tafiti zetu,” amesema Dk Mwasilu na kuongeza:
“Ndaki ya hhandisi na teknolojia ilitokana na kilichokuwa Kitivo cha Uhandisi (FoE) kilichoanzishwa na UDSM mwaka 1973 kwa msaada wa serikali ya Shirikisho la Jamuhuri ya Ujerumani.
“Kitivo cha Uhandisi kilianzishwa ili kutimiza malengo makuu ya kutoa mafunzo ya uhandisi, kufanya utafiti juu ya utumiaji wa maliasili na kutoa huduma za kitaalamu kwa viwanda, serikali, na mashirika binafsi na umma kwa ujumla.
Amesema llipoanzishwa kitivo hicho kulikuwa na idara tatu ambazo ni Uhandisi Ujenzi, Uhandisi Umeme na Uhandisi Mitambo mwaka 1978/79.
” Mwaka 1984 taasisi ya ubunifu wa Uzalishaji (IPI) ilianzishwa kwa lengo la kubadilisha matokeo ya tafiti zilizofanywa na FoE na kuundwa kwa teknolojia inayofaa kutumika katika maeneo ya vijijini katika nyanja kama vile mashine za kilimo, usindikaji na uchimbaji wa mazao ya kilimo, uchimbajidogo wa madini, nyumba za gharama nafuu na mifumo ya nishati endelevu,”amesema