NA MWANDISHI WETU, DAR ES SALAAM
HOSPITALI ya Taifa ya Muhimbili (MNH) inapokea watoto 500 kila mwaka ambao ni wagonjwa wapya wa ugonjwa wa saratani ambapo pia kati ya Aprili 2021 hadi Aprili 2023 watoto 199 walipoteza maisha.
Aidha Duniani kwa ujumla kila mwaka visa vipya vya saratani 400,000 vinagundulika huku ukanda wa Jangwa la Sahari maambukizi mapya kwa mwaka ni watu 40,000.
Hayo yamesemwa Mei 1, 2023 jijini Dar es Salaama na Mkurugenzi Mtendaji Hospitali ya Taifa Muhimbili(MNH) Prof Mohhamed Janabi wakati wa ufunguzi wa Mafunzo kwa wauguzi kuhusu namna ya kuwahudumiwa watoto na vijana wenye saratani.
Prof. Janabi watu wengi wanajua saratani iko kwa watu wazima tu kumbe pia saratani ziko kwa watoto na Muhimbili kuna kitengo kikubwa chenye vitanda zaidi 30 katika jengo la watoto.
“Na hapa nazungumzia saratani zote kuanzia ya damu ,mapafu,mifupa,ini na zingine kwahiyo mafunzo kama haya ni muhimu kwasababu mtoto mwenye saratani huduma zao ziko tofauti kama mgonjwa akija na homa,”alisisitiza Prof Janabi.
Alisema Mafunzo hayo yanahusisha wauguzi kutoka nchi za Tanzania,Malawi,Ethiopia,Uganda,Rwanda na Kenya.
“Leo tunafungua mafunzo ya magonjwa ya saratani kwa watoto na vijana tunafanya pamoja na wenzetu wa Uingereza ambao ni wadhamini wakuu na sisi Muhimbili ndo wenyeji wao Mafunzo haya yanafanyika kwa mara ya kwanza nchini na yanahusisha wauguzi kutoka nchi sita,”alieleza.
Alisema Wauguzi hao watachukua mafunzo na kuwafundisha wauguzi wengine katika nchi zao.
“Wanafundishwa jinsi dawa zinavyofanya kazi na jinsi ya kuwahudumia kama wauguzi na wao pia watatoa kwa wauguzi wenzao kuwasimamia watoto.
Prof Janabi alisema mafunzo hayo ni muhimu na yamekuwa yakifanyika mara ya nne sasa kwa wakufunzi na wanafunzi wanatoka nchi hizo ambao pia watakuwepo kwa siku nne na watatembea hospitali ya Taifa na Ocean Road.
Aliishukuru serikali kwa kuendelea kusaidia kwenye vifaa na dawa kwani gharama ni kubwa.
“Lakini tunashukuru kwa msaada kwani wengi wa watoto wanatoka katika familia zisizo na uwezo mkubwa na hata wale wenye uwezo wa katika dawa ni ghali na vipimo hivyo bado gharama ni kubwa,”alieleza na kuongeza
“Kwa msaada wa serikali tunapata baadhi ya dawa naishukuru Taasisi ya Uingireza ukipata elimu ni silaha kubwa katika matibabu ya watoto na mwakani watoe sisi tuko tayari muda wote.
Alisema Saratani zingine mtu unaweza kujikinga na pia kumuwahisha mtoto hospitali ni muhimu kwani anaweza kupata matibabu na kupona kabisa.
Kwa upande wake Mgeni rasmi katika kufungua mafunzo hayo,Mkurugenzi Msaidizi Huduma za Kitabibu za Uuguzi na Ukunga Paul Magesa alisema wizara inajukumu la kushughulikia tatizo na kulimaliza na kwa sehemu nyingi serikali imeelekeza nguvu kwenye kuzuia badala ya kutibu.
Alisema Serikali ya Samia imewekeza kwenye miundombinu nchi nzimaa ambapo imejenga hospitali za mikoa inaweza kutoa hudumia kwenye saratani kwa ujumla na pia kuna hospitali ya Ocean Road,Muhimbili,Bugando,Benjamini Mkapa hivyo inazidi kupanua wigo wa huduma.
“Inahakikisha huduma zinawafikiwa watanzania kwa kadiri inavyowezekana lakini pia tumekuwa na mafunzo kwenye vyuo vikuu na awali kulikuwa hakuna wauguzi wanafundishwa kuhudumia wagonjwa wenye saratani sasa wapo kwenye ngazi ya shahada na shahada ya uzamivu tunazidi kuhamasisha hospitali kuwaruhusu kusoma na kurudi katika vituo vya kazi kuhudumia watanzania,”alisisitiza.
Naye Muuguzi kutoka Hospitali ya Kenyata iliyopo nchini Kenya,Beatrice Amadi anayehudumia watoto wenye saratani alisema changamoto ni mafunzo upande wa wauguzi kwa kuhuduma watoto kwani wamesahaulika kidogo kuhusu elimu kwa wauguzi .
“Wameachwa nyuma kiasi na sasa tunaanza kuamka na kujua watoto wanatakiwa kuhudumiwa nesi wakipata elimu wataweza kuwahudumia na kuwasaidia waweze kuishi kama kutoa dawa za kupunguza maumivu tukipata ujuzi watoto wataishi,”alibainisha.
Alisema changamoto nyingine ni Jamii haifahamu saratani kwa watoto na wengi wanafikiria kuwa hawaweze kupata wanaenda ngazi za chini na hawatambuliki wanafika hatua ya juu ikiwa umeshakua inakuwa ngumu kutibika.