NAIROBI, KENYA
RAIS Mstaafu wa Kenya, Uhuru Kenyatta ameondolewa kuwa kiongozi wa chama cha Jubilee na upande hasimu unaomuunga mkono Rais William Ruto, kufuatia mgogoro unaoendelea ndani ya chama hicho huku ikidaiwa muda wa kiongozi huyo umefikia kikomo.
Hivi karibuni kumeibuka makundi mawili hasimu ndani cha chama hicho huku moja likimuunga mkono mkono rais mstaafu Kenyatta, wakati kundi jengine likishikamana na utawala wa sasa wa Rais Wiliam Rutto.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotelewa na upande unaoongozwa na Kaimu Katibu Mkuu wa Jubilee, Kanini Kega, umesema umemuondoa madarakani rais huyo wa zamani na nafasi yake kuchukuliwa na Mbunge mteule Sabina Chege.
Kwa mantiki hiyo, Mbunge Chege atakuwa kiongozi wa muda wa chama hicho, hata hivyo; mchakato wa wa kumrithisha nafasi hiyo uko unaendelea.
Akitoa tangazo hilo, Kega ambaye pia ni Mbunge wa Bunge la Afrika Mashariki, amesema uamuzi wa kumvua madaraka ya kiongozi wa chama rais mstaafu Kenyatta, ulitolewa na Baraza Kuu la Kitaifa la Jubilee katika mkutano uliofanyika mapema leo Jumanne.
“Ofisi ya kiongozi wa chama imetangazwa kuwa wazi na sasa Sabina Chege atakuwa Kaimu Kiongozi wa Chama cha Jubilee,” Kega alisema wakati wa mkutano na wanahabari.
Kega alisema kikao cha NEC ambacho kilihudhuriwa na wajumbe 22 kati ya 28, kilifanya uamuzi baada ya Uhuru kudaiwa kukiuka katiba za chama na sheria za nchi.
Alitoa mfano wa Sheria ya Kustaafu na Mafao ya Rais ambayo inamzuia Uhuru kushika nafasi ya uongozi katika chama miezi sita baada ya uchaguzi.
Uhuru alipaswa kujiuzulu wadhifa wake wa chama kufikia Machi 13, ikiwa ni miezi sita baada ya kukabidhi mamlaka kwa Ruto.
“Kiongozi huyo wa zamani wa chama pia amejiendesha vibaya kwa kutoa matamshi kwa niaba ya chama,” alisema na kuongeza kuwa mwenendo wa Uhuru umepelekwa kwa kamati ya nidhamu ya chama.
“Suala la utovu wa nidhamu linapelekwa kwenye kamati ya taifa ya nidhamu kwa hatua zaidi,” alisema.
Kwa mfano, Kega alisema Uhuru amekiuka katiba ya chama kwa kuitisha Kongamano la Wajumbe wa Kitaifa la Mei 22 kupitia maazimio ya NEC yaliyohudhuriwa na wajumbe saba pekee.