NA JULIETH RAMADHANI, PWANI
JESHI la Polisi mkoani Pwani limesema mtu mmoja amekufa na wengine watatu wamejeruhiwa baada ya gari dogo walilokuwa wakisafiria kugonga lori lililokuwa limesimama pembezoni mwa barabarani.
Kamanda wa Polisi wa mkoa huo, Pius Lutumo amewaeleza waandishi wa habari ofisini kwake mjini Kibaha kuwa ajali hiyo ilitokea jana saa 12:45 asubuhi katika Kijiji cha Chamakweza kwenye Wilaya ya Kipolisi Chalinze.
Kamanda Lutumo alisema marehemu na majeruhi walikuwa wakitoka Dar es Salaam kwenda Morogoro wakitumia gari aina ya Toyota Prado lenye namba za usajili T 548 DSZ likiendeshwa na Abubakar Hadingoka (21) mkazi wa Morogoro.
Alisema gari hilo liligonga kwa nyuma gari lenye namba za usajili T 746 AKZ aina ya Scania lenye tela namba T 673 AEV likiendeshwa na Stanslaus Mbarahe (34) mkazi wa Dar es Salaam.
“Aliyefariki ni Lilian Munisi ambaye ndiye mmiliki wa gari aina ya Prado na ni mfanyabiashara wa Morogoro na majeruhi ni dereva Hadingoka, Moses Tenganamba (25) na Grace Rwengisa (25) wote wafanyabiashara wa Morogoro,” alisema Kamanda Lutumo.
Alisema chanzo cha ajali hiyo ni uzembe wa dereva wa gari dogo kushindwa kulimudu na kuligonga kwa nyuma lori lililokuwa limeegeshwa pembezoni mwa barabara.