NA MWANDISHI WETU, MLELE
HALMASHAURI ya Wilaya ya Mlele Mkoa wa Katavi leo Aprili 24, 2023, imeanza maadhimisho ya miaka 59 ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar kwa kufanya shughuli mbalimbali ikiwemo usafi, kuzindua vyumba vya madarasa shule ya Sekondari Inyonga na kufanya kongamano la michezo mbalimbali.
Mapema leo akizungumza na wananchi wa mji wa Inyonga wakati wa kufanya usafi kituo cha Afya Inyonga B mwakilishi wa mkuu wa Wilaya ya Mlele, Lincolin Tamba amewataka wananchi wilayani humo kudumisha umoja na mshikamano kama ilivyo nia ya waasisi wa Muungano huo, hayati Baba wa Taifa Mwalimu Julius Nyerere na hayati Abeid Amani Karume Rais wa Kwanza wa Zanzibar.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Halmashauri ya Mlele, Soud Mbogo, amesema Muungano unafaida nyingi kisiasa na kiuchumi, ambapo wananchi kutoka Zanzibar wanajiinua kiuchumi kwa kufanya shughuli zao Tanzania Bara bila bughudha yeyote, pia ipo hivyo kwa wananchi wa Tanzania Bara wanafanya shughuli zao Zanzibar.
Naye Kaimu Mkurugenzi Mtendaji Halmashauri ya Mlele, Habiba Mtunguja, amesema si jambo dogo kwa Muungano kufikisha miaka 59, hivyo ni jukumu la kila mwananchi kujivunia na kuulinda.
Kimkoa kilele cha maadhimisho hayo kitafanyika Halmashauri ya Wilaya ya Mpimbwe Aprili 26, 2023, ambapo mgeni rasmi anatarajiwa kuwa Mkuu wa Mkoa wa Katavi Mwanamvua Mrindoko.