NA ANTHONY SOLLO , DODOMA
SERIKALI imesema Ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG)itafanyiwa kazi bila woga ili kulinda rasilimali za watanzania.
Kufanyiwa kazi kwa ripoti kunakuja kutokana na mijadala inayoendelea nchini hivyo wananchi hawapaswi kuwa na hofu.
Kauli hiyo imetolewa na Msemaji Mkuu wa Serikali na Mkurugenzi wa Idara ya Habari Maelezo Gerson Msigwa jijini Dodoma Aprili 19, 2023 katika dhifa ya Iftar.
Msigwa amewataka wananchi kuachana na mijadala kuhusu Ripoti badala yake wajikite kwenye ujenzi wa Taifa .
“Niwatoe hofu wananchi, ripoti ya CAG ni nyenzo inayotumiwa na Serikali kusimamia rasilimali za watanzania,hivyo niwahakikishie kupitia ripoti hiyo Serikali ipo macho kulinda na kutetea rasilimali,achaneni na taarifa za mitandaoni zinazokatisha tamaa,”amesema Msigwa.
Kuhusu Miradi ya kimkakati Msigwa amesema mwendo ni uleule hakuna kilichobadilika wala kusimama na kutolea mfano Mradi wa Reli Morogoro -Makutopora kuwa unaendelea kutekelezwa ukiwa umefikia asilimia 93.3.
“Miradi yote ya kimkakati inaendelea kutekelezwa, Serikali ya Rais Dk Samia Suluhu Hassan ina nia ya dhati na itahakikisha mipango yote inatekelezwa ikiwemo mabehewa ya ghorofa,mradi wa uzio wa tembo ambao umeanza Kwa mara ya kwanza nchini na barabara ya mzunguko ya Dodoma ambayo imefikia asilimia 18.
Kama ilivyo kwa viongozi wengine katika kipindi hiki cha mwezi mtukufu wa Ramadhani,Msemaji wa Serikali pia ametumia nafasi hiyo kuwataka Waandishi wa Habari na watanzania kwa ujumla kuendelea kutendeana mema na kuepuka chuki na majungu miongoni mwao.
“Kiu yangu kila siku ni kuona mnashirikiana,mnapendana na kusaidiana,tukiishi Kwa upendo tunakuwa na utulivu unaotufanya tuwe na bidii Katika ujenzi wa Taifa lefu,tuheshimiane siku zote kwa kuzingatia miiko na maadili ya nchi yetu,”amesisitiza Msigwa.