NA MWANDISHI WETU, DAR ES SALAAM
WIZARA ya afya imepokea msaada wa majokofu 390 kutoka ubalozi wa Japan .
Aidha Shirika la Vodafone limetoa msaada wa ukarabati wa vyumba sita kuimarisha mnyororo wa baridi yenye thamani ya Sh.Milioni 690 kwa ajili ya mchakato wa kuhifadhia chanjo hizo.
Msaada huo wenye thamani ya Sh.bilioni 3.27 utasaidia kuhifadhia chanjo za Saratani ya mlango wa kizazi, Uviko-19 pamoja na chanjo za watoto.
Majokofu hayo yenye uwezo wa kuhifadhi ubaridi kwa siku tano pindi umeme unapokatika tayari yameanza kusambazwa katika mikoa 13 Tanzania bara na yatatumika kuhifadhia chanjo za Saratani ya mlango wa kizazi, Uviko-19 pamoja na chanjo za watoto.
Akipokea msaada huo kutoka kwa balozi wa Japan nchini, Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu amesema kipaumbele cha wizara hiyo kwa sasa ni utoaji wa chanjo hususani kwa watoto kutokana na tafiti mbalimbali kuonyesha dola moja inayowekezwa katika chanjo huokoa dola 20 hadi 44 kwenye matibabu.
“Tunahitaji majokofu ya kisasa 5,822 tayari Serikali tumeshanunua 2,012 hayo mengine yaliyobaki tutaendelea kununua na kushirikiana na Shirika la Watoto Duniani (Unicef),” amesema.
Waziri Ummy ametaja mikoa itakayonufaika na majokofu hayo ni Arusha, Dar es Salaam, Lindi, Mtwara, Shinyanga, Simiyu, Singida, Dodoma, Katavi, Rukwa, Tabora, Kigoma, Songwe na Zanzibar.
“Nitoe rai kwa wananchi kuendelea kutumia huduma zetu za chanjo ambazo zinapatikana nchi nzima ili kuhakikisha watoto watoto wanapata chanjo kwa mujibu wa ratiba, hii Itasaidia kukinga nchi yetu didi ya mlipuko wa magonjwa yanayozuilika,”amesema.
Kwa upande wake balozi wa Japan-Tanzania, Yashushi Misawa amesema msaada huo ni muendelezo wa misaada ambayo nchi yake inatoa kwenye sekta ya afya ambapo tayari Japan kupitia mpango wa COVAX imetoa dola milioni 30 kwa nchi za Afrika na Amerika kuhamasisha chanjo hasa ya Uviko-19.
Akizungumzia ukarabati wa nyumba za kuhifadhia mnyororo wa baridi, Mkurugenzi wa Fedha Vodacom Hilda Bujiku amesema msaada huo wameutoa kunisaidia Serikali kufikisha upatikanaji wa chanjo ya salama.
Naye Meneja wa Mpango wa Taifa wa Chanjo Dk Florian Tinunga msaada huo unaipa uwezo wa kuhifadhia chanjo zote eneo moja badala ya kuzipeleka Bohari Kuu ya Dawa (MSD).