NA MWANDISHI WETU, DAR ES SALAAM
ALIYEKUWA Mgombea Ubunge Jimbo la Mbagala 2020 kwa tiketi ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) ‘Mbunge wa Wananchi’ Khadija Mwago almaarufu kama Waukae Nyamwago ametembelea kituo cha kulelea watoto yatima kijulikanacho kwa jina la Arafa kilichopo Mapunda Kata ya Chamazi nje kidogo ya jiji la Dar es salaam.
Kabla ya ziara ya Aprili Mosi, 2023 Mbunge Mwago alifanya ziara ya kujua mahitaji ya kituo hicho Machi 28, 2023 ambapo alikutana Kiongozi wa Kituo cha Arafa Ustadhati Fatuma na makundi ya watu mbali mbali
Aidha katika ziara hiyo Mbunge huyo aliombwa na mlezi wa kituo hicho Ustadhati Fatuma ashirikiane nao kupata mahitaji maalum kwa watoto hao yatima hususani wakati huu wa mwezi mtukufu wa Ramadhani.
Baada ya ziara hiyo ya Machi 28, 2023 , Aprili Mosi , 2023 Mbunge huyo kwa kushirikiana na wadau wengine wameweza kufanikisha baadhi ya mahitaji yaliyoombwa.
Katika ziara hiyo Mwago ameongozana na Kamanda wa Operesheni wa Jimbo la Mbagala Fatma Thabiti pamoja na aliyekuwa kampeni meneja na mratibu mkuu wa shughuli za uchaguzi jimbo la Mbagala 2020 Herman Kiloloma
Pamoja na mambo mengine, Mwago ametumia ziara hiyo kuendelea na maandalizi ya mikutano ya shukrani kwa wapiga kura wa Mbagala itakayoanza April 29, 2023 mara baada ya Mfungo wa Mwezi Mtukufu kumalizika.