NA MWANDISHI WETU, DODOMA
TAASISI ya Elimu Tanzania, (TET) na Tume ya Taifa ya Kudhibiti Ukimwi, (TACAIDS) wameendesha mafunzo kwa Wadhibiti Ubora na Maofisa Elimu Kata wa Halmashauri za Wilaya tatu za Mkoa wa Dodoma za Mpwapwa, Dodoma jiji na Chamwino ambapo mafunzo hayo ya siku Tano, yameanza rasmi leo Machi 27.
Mafunzo hayo kwa ajili ya kupata uzoefu wa utekelezaji wa shughuli za elimu na afya katika kuunda, kusimamia, kutoa taarifa na kuratibu shughuli za Mradi wa Timiza Malengo.
Akifungua mafunzo hayo Mkurugenzi wa Halmashauri ya Chamwino, Dk. Semestatus Mashimba amewataka washiriki hao kufuata miongozo ya ufundishaji, maadili ya Kitanzania pamoja na tamaduni ili kukabiliana na wimbi la mmomonyoko wa maadili.
“Hakikisheni mnafuatilia vyema mafunzo haya ili mkienda kwenye ufuatiliaji mkasaidie kuondoa mmomonyoko wa maadili yetu hasa kwa vijana nchini” amesema Dk. Mashimba.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Mafunzo ya Mitaala wa TET, Dk. Fika Mwakabungu amesema kuwa mafunzo hayo yatasaidia kukuza uelewa wa pamoja kuhusu elimu ya Stadi za Maisha zinazolenga Afya ya Uzazi, VVU/UKIMWI na Jinsia, kuwezesha ufuatiliaji wa utekelezaji wa mitaala kwa kulenga mafunzo yaliyotolewa kwa walimu kuhusu maudhui lengwa katika ngazi ya darasa.
Pia watajenga mtazamo chanya katika kuwahamasisha walimu, wanafunzi na vijana katika jamii kuzingatia misingi ya afya ili kupunguza maambukizi ya magonjwa kwa ustawi wa nguvu kazi ya vijana.
Aidha, Mratibu wa Mafunzo wa TACAIDS, Kelvin Kisoma amesema kuwa, mafunzo hayo yatasaidia washiriki kuongeza uelewa na kuwa namna bora ya kusimamia, kuratibu na kufanya ufuatiliaji wa utekelezaji wa maudhui ya stadi za Maisha inayozingatia afya ya uzazi,VVU na UKIMWI na ukatili wa kijinsia
Jumla ya Halmashauri 18 nchi nzima zitafikiwa katika kuhakikisha elimu hiyo inawafikia walengwa ambao ni wanafunzi nchini huku Halmashauri za Geita na Chato zikitarajia kupata mafunzo hayo wiki ijayo.