NA MWANDISHI WETU, MWANZA
MKAZI wa Mtaa wa Ihira, Kata ya Buhongwa mkoani hapa, David Deogratius (32) ameuawa na wananchi wenye silaha za jadi baada kudaiwa kuiba runinga nyumbani kwa mwalimu wa Shule ya Msingi Kirumba.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza, Wilbroad Mutafungwa amesema tukio hilo limetokea Jumamosi 25, 2023 na kufafanua kwamba hata hivyo mtuhumiwa huyo alifariki dunia wakati akipatiwa matibabu.
Amesema mtuhumiwa huyo inadaiwa baada ya kuiba runinga (flat screen) aliruka dirishani ndipo wananchi walipomuona na kumvamia. Pia miongoni mwa vifaa alivyokutwa navyo ilikuwa ni nyundo, bisibisi na spana ambavyo inaelezwa alivitumia kwenye shughuli zake za kihalifu.
Askari waliokuwa doria walifika eneo la tukio kisha kumnusuru na kumuwahisha Hospitali ya Bugando kwa ajili ya matibabu.
Kamanda ACP Mutafungwa amesema baada ya kupitia kumbukumbu zake za kiuhalifu, wamebaini kwamba alitoka Gereza la Butimba Machi 22, mwaka huu.
“Alitoka kwa dhamana na awali alikuwa akishtakiwa kwa kosa la wizi ambalo kesi yake ya jinai ndiyo ilikuwa imemuweka hapo gerezani,” amefafanua.
Kamanda Mutafungwa amesema mtuhumiwa huyo enzi za uhali wake alitoka gerezani Machi 22, 2023 na kukaa uraiani siku moja, kisha kuangukia kwenye tukio jingine la wizi lililosababisha kupigwa na wananchi.
“Niwatahadharishe wahalifu wanaopata dhamana, kama mtu ametuhumiwa na kosa la kijinai, anapokuwa nje anatakiwa kuendelea kuwa raia mwema. Asijihusishe kabisa na vitendo vya kihalifu. Hata hivyo Jeshi la Polisi tunawatafuta watu waliofanya tukio hilo la kujichukulia sheria mkononi,” amesisitiza.
Wakati huo huo, Kamanda Mutafungwa ametoa onyo kwa wananchi wote wenye tabia ya kujichukulia sheria mkononi badala yake wanapopata taarifa za uhalifu wa aina yeyote ile kutoa taarifa kwa Jeshi la Polisi.