NA MWANDISHI WETU, DODOMA
WAZIRI wa Uwekezaji, Viwanda na Biashara Dk. Ashatu Kijaji amewakaribisha wawekezaji kutoka nchini Urusi kuja kuwekeza Tanzania katika sekta ya Viwanda, Biashara, Kilimo, Utalii, Uvuvi, Madini, Mawasiliano, usafiri na ujenzi.
Dk Kijaji ameyasema hayo alipokutana na kufanya mazungumzo na Andrey Avetisyan Balozi wa Urusi nchini Tanzania walipokutana katika ofisi ya Waziri iliyopo jengo la PSSF jijini Dodoma.
Dk. Kijaji amesema kuwa ushirikiano uliopo baina ya Tanzania na Urusi ni wa muda mrefu hasa katika ushirikiano wa kisekta kupitia tume ya pamoja ya biashara na ushirikiano wa kiuchumi baina ya Tanzania na Urusi kuwekeza katika miradi mbalimbali hivyo hii ni fursa ya kuwaunganisha watanzania kuwekeza katika kuzalisha bidhaa zinazohitajika Urusi.
Balozi wa Urusi nchini Tanzania Avetisyan amesema kuwa Urusi na Tanzania ni marafiki na ndugu wa muda mrefu hasa katika eneo la ufanyaji biashara na kwa sasa nchi ya Urusi imewekeza nguvu kubwa katika kuongeza mashirikiano na bara la Afrika na Tanzania ni Nchi mojawapo ambayo mazingira yake ya uwekezaji yameimarika kutokana na Uongozi uliopo wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan.
Avetisyan ameongeza kuwa Urusi imeandaa Mkutano wa majadiliano ya Biashara na Uchumi utakaoshirikisha nchi za Afrika (Russian African Summit on Business and Economic) unaotarajiwa kufanyika nchini Urusi mwezi Julai, 2023 ambapo Tanzania ni mojawapo ya Nchi itakayoshiriki Mkutano huu.